KAMISHNA Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Rogers Sianga alisema wamedhibiti uingizaji wa dawa za kulevya nchini na hali kwa sasa si kama ilivyokuwa siku za nyuma huku akifichua kuwa mzee wa miaka 80 wamemdaka akijihusisha na biashara hiyo haramu.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Sianga alisema wamebaini mbinu nyingi wanazotumia wasafirishaji hao wa dawa za kulevya kwa kutumia wazee:
“Tumebaini wanatumia wazee wa hadi miaka 80 na watu wa nje kusafirisha… kuna babu mmoja wa miaka 80 alikamatwa akiwa na dawa za kulevya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” alibainisha kiongozi huyo bila kumtaja jina.
Kamishna Mkuu Sianga alisema kwa sasa wamebaini kuwa baada ya ulinzi kuimarishwa katika viwanja vya ndege na ukanda wa bahari ya Tanzania, wasafirishaji wa dawa hizi wameanza kutumia pwani ya Msumbiji kisha kusafirisha kwa njia za panya kuingia nchini kwa kutumia magari na pikipiki.
Sianga alisema tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo wasafirishaji walikuwa wakitumia zaidi watu waliokuwa wakimeza dawa hizo kuanzia nusu kilo hadi kilo mbili, kwa sasa wasafirishaji wanatumia njia ya kuficha dawa hizo katika mabegi na mizigo na kusafirisha kwa njia ya ndege na majahazi.
Related image
“Lakini zaidi tumebaini kwamba wasafirishaji wamekuwa wakichukua vijana hapa na kuwapa mafunzo, kisha kuwapeleka Afrika Kusini, Angola na Msumbiji ambako huwabebesha mizigo na kuondokea huko,” alisema kamanda huyo.
Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa ushirikiano baina ya mamlama yake na vyombo vya ulinzi vya kimataifa ikiwemo Indian Ocean Forum on Maritime Crimes mwaka 2010 na baadaye Combined Maritime Forces/ CTF 150 vinavyohusisha muungano wa majeshi ya nchi mbalimbali katika Bahari ya Hindi vilivyoanzishwa kudhibiti uharamia, imesaidia ukaguzi wa meli na kupungua kasi ya usafirishaji wa dawa za kulevya katika pwani ya bahari hiyo.
Tangu kuingia madarakani kwa Sianga, upatikanaji wa madawa hayo ya kulevya nchini umepungua sana, kuonesha kuwa biashara hiyo haramu inadhibitiwa nchini kwa nguvu kubwa. Hata yale maeneo yaliyokuwa maarufu kwa ‘mateja’ yaani watumiaji wa bidhaa hiyo, wamekuwa hawaonekani kwa sasa, hali inayofanya sehemu hizo kuwa shwari kwa sasa