Mzoga wa mnyama unavyoweza kukupeleka jela
0
October 06, 2018
NA ELBOGAST MYALUKO
Kwa namna moja ama nyingine neno Nyara za serikali linaweza kuwa linatumika tu katika maisha ya kawaida pengine bila kujua undani wake, lakini wakili wa kujitegemea Bashir Yakub amefafanua zaidi.
Kupitia MJADALA wa EATV leo Oktoba 5, 2018 Yakub amesema wanyama wote wa porini pamoja na ndege na wadudu kama nyoka wanaweza kukutia hatiani endapo utakutwa nao nyumbani kwani hizo zote ni nyara za serikali.
''Unajua nyara za serikali haziishii tu kwa wanyama wa porini kama ilivyozoeleka au wakiwa hai tu, haijalishi wawe ni wadudu au hata kama ni mzoga wa Simba au mnyama yoyote, huruhusiwi kukaa nao kwani ni kosa kisheria na sheria haina kipengele cha kwamba hukujua'', amesema.
Aidha ameweka wazi kuwa makosa yanayohusu nyara hizo yamegawanyika katika mitindo tofauti ambayo ni kumiliki, kuuza na kununua nyara hizo bila kuwa na kibali au leseni ambayo hutolewa na Rais.
Adhabu za makosa hayo zimeainishwa kutokana na thamani ya nyara ulizokutwa nazo akitoa mfano kuwa kwa nyara zenye thamani ya shilingi laki moja mtuhumiwa anaweza kwenda jela hadi miaka mitano.
Yakub ameitaka jamii kuwa makini na nyara za serikali kwasababu sheria mpya ina makali kuanzia kwa anayemiliki hadi kwa yule anayejua mtu flani anamiliki na asitoe taarifa naye anakuwa amefanya kosa.
Tags