Kwa muda mrefu nchi ya Ethiopia, ilikuwa ikitawaliwa kwa mabavu tangu enzi za utawala wa Mengistu Haile, ambaye alipinduliwa mwaka 1991.
Ethiopia ilipaa kiuchumi, hasa kipindi cha utawala wa Waziri Mkuu Meles Zenawi, lakini bado kulikuwa hakuna demokrasia ndani ya taifa hilo katika kipindi cha utawala wa huo tangu alipoongoza Serikali ya mpito kati ya 1991-1995 na baada ya kutwaa madaraka kamili, mwaka 1995 mpaka kifo chake 20 Agosti 2012.
Baada ya Meles Zenawi, Waethiopia walidhani kuwa wataweza kupumua, lakini haikuwezekana. baada ya aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa Zenawi, Haile Mariam Desalegn kushika hatamu naye aliendeleza utawala wa kibabe.
Kwa kawaida binadamu hata aliye hiba, usipompa uhuru, basi utaingia matatani. Uhuru wa kufikiri na kusema, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kupashana habari bila kuletewa kipingamizi, uhuru wa kukosoa watawala bila kuingia matatani. Naam huyo ndiyo binadamu na hizo ndiyo hulka zake ambazo watawala wengi wa Afrika wamekuwa wakizipuuza.
Watawala wa Ethiopia, kwa muda mrefu, waliwabana wananchi, lakini Desalegn, alizidiwa na ‘nguvu ya umma’. Dalili za kuzidiwa zilianza kuonekana mwaka 2015, palipozuka maandamano makubwa dhidi ya serikali katika Jimbo la Oromia. Serikali ilitumia jeshi kuzima maandamano hayo na watu 75 walipigwa risasi na kupoteza maisha, lakini maandamano hayakukoma.
Wananchi walizidi kupatwa na jazba hadi kufikia Agosti 5, 2016 nchi nzima ilikuwa ni maandamano. Siku hiyo majeshi ya serikali yaliwauwa wananchi 50. Hali ikawa tete zaidi kwani waandamanaji hawakurudi nyuma katu.
Kufikia mwezi Aprili 2017, jeshi lilituhumiwa kuwaua zaidi ya waandamanaji 700, lakini umma haukurudi nyuma hadi Februari 2018, Desalegn alipoamua kuacha mageuzi yachukue na kung’atuka kabla ya hayajamkuta yaliyomkuta Mengistu.
Kufikia Aprili 2, 2018, Waethiopia waliutangazia ulimwengu kuwa Waziri Mkuu mpya, Dk. Abiy Ahmed Ali, ndiye atakaye kuwa kiongozi wa nchi hiyo yenye uchumi unaokuwa kwa kwa asilimia 10, kwa muongo mmoja sasa.
Dk. Abiy Ahmed (42), ni kiongozi wa chama cha Oromo Peoples’ Democratic Organization (OPDO), ambacho ni moja ya vyama vinne vinavyounda Chama cha Ethiopia Peoples’ Revolution Democratic Front (EPRDF), ambacho pia Waziri Mkuu Dk. Abiy Ahmed ni Mwenyekiti pia.
Kwa muda mfupi ambao Dk. Abiy Ahmed amekaa madarakani, ni dhahiri shahiri ameonesha nuru kwa Waethiopia na Afrika kwa ujumla, kwani amefanya mageuzi ambayo umma wa Ethiopia ulikuwa ukiyapigania kwa jasho na damu kwa siku nyingi.
Abiy Ahmed, ameruhusu uhuru wa maoni na kukosoa serikali, pia amevionya vyombo vya dola kutowaonea wananchi wanaoikosoa serikali, kwani wao ndiyo chanzo cha mamlaka.
Pia Dk. Abiy Ahmed ameachia wafungwa wengi wa kisiasa ndani ya Ethiopia, pia ameviachia huru vyombo vya habari zaidi 240 (Televisheni, Redio, Magezeti, Blogs, mitandao mbalimbali ya habari) ambavyo vilifungwa na mtangulizi wake.
Mwezi Mei, Dk. Abiy Ahmed aliamuru wafungwa 7,600 katika Mkoa wa Oromo kuachiwa huru pia, Mei 29, 2018, kiongozi wa kundi la Ginbot 7, Andargechew Tsege, aliachiwa kwa amri ya Rais wa Ethiopia pamoja na Muluta Teshome na wafungwa wengine wapatao 575.
Ikumbukwe Ethiopia kiongozi mwenye nguvu ni Waziri Mkuu, ingawaje wa Rais kama ilivyo kwa Israel na Ujerumani, kansela ndiye mwenye nguvu. Andargechew Tsege na wenzie, walikuwa wakituhumiwa kwa makosa ya ugaidi ambapo kesi hiyo walibambikiziwa kwa kuwa walikuwa wanawakosoa watawala bila woga.
Dk. Abiy Ahmed hakuishia tu ndani ya Ethiopia, bali alikwenda mbali. Kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 20, Kiongozi Mkuu wa Ethiopia alizuru nchi jirani ya Eritrea ambayo imekuwa katika mgogoro na Ethiopia kwa muda mrefu licha ya kuwa na majadiliano na makubaliano yakumaliza tofauti zao (Ethiopia-Eritrea War, Algiers Agreements 2000), ambapo watawala wa Ethiopia wamekuwa wakiyapuza, lakini Abiy Ahmed ameyakubali baada ya kuzuru Eritrea Julai 8, 2018 na kutiliana saini na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki.
Hadi sasa Ethiopia na Eritrea wameshaondoa majeshi yao katika mpaka unaozitenganisha nchi hizo, na Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopia Airlines) limeanza safari zake kutoka Addis Ababa hadi Asmara, Eritrea. Pia Rais Isaias tayari ameshatembelea Ethiopia na kufungua ‘upya’ ubalozi wa Eritrea jijini Addis Ababa.
Kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika kuwa watawala wa Afrika hawawezi kumaliza migogoro yao, bila uongozi wa mataifa ya Magharibi yakiongozwa na kiranja wao Marekani na Uingereza.
Kwa muda mrefu mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, yalikuwa yakiituhumu Eritrea, hasa Rais wake Isaias Afwerki, wakidai ni mbabe/dikteta, lakini kwa hatua hiyo, sasa ni dhahiri Ethiopia na Eritrea za kidikteta, zimefika kikomo.
Ukiachana na makubaliano waliyotiliana siani mjini Asmara, Julai 9, 2018 ya kumaliza uhasama, pia Abiy Ahmed na mwenzie Isaias Afwerk, wametiliana saini makubaliano mengine ya kudumisha amani katika eneo lao na duniani kwa ujumla, kufuatana na mapatano ya Jeddah nchini Saudi Arabia, mnamo tarehe Septemba 16, 2018 mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, Mfalme wa Saudi Arabia, Salman Abudul Aziz, na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki. Ahmed ameamua kuja tofauti na watangukizi wake, na anaonekana kama mkombozi wa Waethiopia.
Kwa wasio jua ni kwamba, Dk. Abiy Ahmed, Shahada yake ya Uzamivu (PhD) alihitimu mwaka jana katika Chuo Kikuu Cha Addis Ababa, Katika Taasisi ya Masomo ya Ulinzi na Amani, tasnifu (Thesis) yake ilihusu masuala ya upatanishi wa migogoro ya Kijamii, Dk. Abiy Ahmed alichapisha tasnifu yake ya “The Social Capital and Its Role in Traditional Conflict Resolution in Ethiopia: The Case of Inter-Religious Conflict in Jimma Zone State”—hivyo sasa yupo ‘field’ baada ya kutoka darasani.
Pia Abiy Ahmed amedhamiria kuifanyia marekebisho Katiba ya Ethiopia ambayo ilikuwa ninawapa watawala madaraka makubwa ambayo waliyatumia vibaya. Anataka kurejesha mamlaka kwa umma, kwani umma ndiyo wenye kuamua hatma ya nchi, na si kikundi cha watawala.
Katika uchumi, Abiy Ahmed amedhamiria kuleta sera ya ubinafsaji, hasa mashirika yote ya umma yanayojiendesha kwa hasara, likiwamo Shirika la Ndege la Ethiopia, licha ya kusifiwa kufanya vizuri, lakini limekuwa mzigo kwa walipa kodi.
Kwa sasa Ethiopia Airlines, ina ndege 100 na hivi majuzi wamezindua safari za Malayasia, lakini bado Abiy Ahmed anaona shirika hilo libinafisishwe, ili kuipunguzia mzigo serikali.
Kwa hayo machache, nashawishika kuona siku Rais John Magufuli wa Tanzamia, atakapokutana na Abiy Ahmed—sijui ni viunga vya pale Magogoni, au katika Jiji la Addis Ababa—makao makuu ya AU ili wapeane maujuzi mazuri zaidi yakuongoza nchi zetu kwa maana ni viongozi wawili imara wanaongelewa sana kwa sasa Africa
Naisubiri hiyo siku, sijajua ni lini! Lakini natamani siku Magufuli atakapkutana na Abiy Ahmed
NA NDAHANI MWENDA