Nay wa Mitego Apigwa Stop Kuimba Mwenyewe Afunguka A-Z

Nay wa Mitego Apigwa Stop Kuimba Mwenyewe Afunguka A-Z
KWA sasa ukipita kwenye vibanda vya kuchajisha simu, vijiwe vya bodaboda, Bajaj, saluni, daladala au kwenye nyumba binafsi, kwa asilimia kubwa utasikia Ngoma ya Alisema ya mkali Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’. 



Nay amekuja kivingine ambapo kwenye ngoma hiyo ametumia kivuli cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye msemo wake wa ‘Vijana Tuamke’! Lakini wakati gumzo la ngoma hiyo likiwa kila kona, mama yake mzazi amemtaka kuachana na muziki na kuangalia biashara nyingine. Showbiz imemtafuta Nay na kufanya naye Exclusive Interview na katika makala haya anafunguka zaidi;



Showbiz: Ulivyotoa wimbo huu mara tulisikia Basata wamekuita, ilikuwaje?

Nay: Kweli niliitwa na wito wangu ulikuwa ni wa muda mrefu siyo kwa sababu nimetoa ngoma mpya, hapana, niliitwa muda mrefu tu kwa kuwa sikuwepo Tanzania, niliporudi na kutoa ngoma mpya ndiyo nikaenda kusikilizia wito wangu.

Showbiz: Nay tumesikia kuwa mama yako mzazi hataki kabisa uendelee kujihusisha na masuala ya muziki kwako kutokana na matatizo yanayokupata unapotoa nyimbo mpya, lakini umetoa wimbo mpya mwezi huu Oktoba ni kiburi au ni nini?



Nay: Mama yangu hataki nifanye muziki na niendelee kuimba kwa sababu ya matatizo ninayokutana nayo katika kazi zangu kwa sababu mara ya mwisho nilipokamatwa baada ya kutoa Wimbo wa Wapo ndiyo alinikataza, aliniambia niachane na muziki nifanye shughuli nyingine maana nitakuja kufa siku si zangu.

Huu wimbo nimefanya kwa ajili ya wananchi wa Tanzania na mashabiki wa muziki wangu, nimefanya kwa ajili ya hali iliyopo kwa sasa, ninampenda sana mama yangu na huwa ninamsikiliza sana, lakini kwa Wimbo wa Alisema nilijua tu unaweza kuzua balaa (utata), lakini nilipokuwa nikiendelea na kukumbuka kauli ya mama wakati nimeingia studio na kurekodi ndiyo nikaambiwa hebu weka sawa mashairi yako na ndipo nikayapangilia na wimbo ukatoka kama mnavyousikia.



Kwa kuwa nilimuahidi mama kuwa sitafanya muziki anaonikataza, kwa hiyo kwenye huu wimbo najua yeye asingeukubali utoke ndiyo maana nikamwambia mama huu ni wa mwisho naapa.

Showbiz: Kwa hiyo unatuhakikishia katika gemu ya muziki ndiyo byebye au unatuambiaje?

Nay: Haaa…haa! Nadhani mnatakiwa kuongea na mama, akisema sawa nitaendelea, nina watoto wangu bado wanasoma najitoa kwa ajili ya Watanzania wenzangu, najitoa kwa ajili ya watu wanaopenda kusikia kitu kutoka kwa sisi wasanii, lakini nina familia ambayo inanipenda zaidi na ninaipenda zaidi kwa mapenzi na kuonesha kiasi watu wananihitaji zaidi mimi Nay, wanahitajika kuongea na mama Nay, lakini hii imetosha.



Showbiz: Kwa hiyo Nay unatuambia kwamba hufanyi tena muziki au utakuwa unaimba kwa staili nyingine?

Nay: Siyo kwamba sitafanya muziki, kuna dizaini ya muziki ambayo mama yangu hataki kusikia nikifanya hasa nyimbo za harakati kama hizi huwa hapendi kabisa kusikia. Kwenye muziki nitaendelea, lakini kwa nyimbo hizi za harakati ambazo mama yangu hazitaki sitafanya kabisa.

Showbiz: Kwa staili hiyo ya muziki utakayoamua kutoka nayo huoni kama utapoteza mashabiki waliokuwa wanapenda nyimbo zako za harakati ulizokuwa ukiwaburudisha?


Nay: Ni kweli huwa nikitoa nyimbo za harakati huwa mashabiki wanapokea kwa nguvu sana mfano mzuri huu wa Alisema, watu wamepokea kwa nguvu wakati nimekaa kimya muda sana imekuwa ni topiki kila sehemu, lakini namuheshimu sana mama yangu kwa kawaida tu hapa nahisi ana presha hii tu ilivyotoka nilipata wakati mgumu sana katika kumuweka sawa mpaka kuelewa nimepata wakati mgumu sana siyo mimi tu ilifika siku kadhaa sikuweza kurudi nyumbani baada ya kusikia Wimbo wa Alisema ilibidi nimtumie mdogo wangu na mtu wa karibu na mama aweze kuongea naye.



Baada ya kuongea naye ndiyo alijibu kuwa sawa nimesikia wimbo wako na umenikumbusha mbali, lakini anachooomba niwe makini tu.

Showbiz: Basata walikuuliza chochote kuhusiana na wimbo huu?

Nay: Huu wimbo umemgusa kila mtu hata wale ambao wanalinda ugali wao wakiwa kazini kwa kufungia kazi za wasanii, sitegemei kama wataufungia kulingana na maudhui ya wimbo wenyewe hata ukisikiliza.



Showbiz: Inasemekana ulitakiwa kubinafsisha mali zako baada ya kuchukua mkopo benki na kushindwa kulipa, je ni kweli?

Nay: Unajua mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe, nimezushiwa vitu vingi sana, lakini namuachia Mungu tu ndiye anajua, walitangaza pia kuwa Studio ya Free Nation siyo yangu, lakini leo hii mmekuja kunihoji katika studio yangu ambayo kwa uhalisia kama mlishifika hapo nyuma kuna marekebisho makubwa tu, sasa sijui watasemaje tena.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad