Ndege ya kuwabeba abiria ya shirika la Lion Air aina ya Boeing 737 imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege mjini Jakarta, maafisa wa Indonesia wamesema.
Ndege hiyo safari nambari JT-610 iliyokuwa imewabeba abiria 188 ilikuwa safarini kutoka mji huo mkuu wa Indonesia kwenda Pangkal Pinang, jiji linalopatikana katika visiwa vya Bangka Belitung.
Katika kikao na wanahabari, maafisa wamesema ndege hiyo, ambayo ni ndege mpya aina ya Boeing 737 MAX 8, ilikuwa imewabeba abiria 178 watu wazima, watoto watatu, marubani wawili na wahudumu watano wa ndege.
Yusuf Latif, msemaji wa shirika la huduma za uokoaji na kuwatafuta manusura amewaambia wanahabari: "Imethibitishwa kwamba ndege hiyo imeanguka."
Afisa wa shirika hilo la ndege ameiambia BBC kwamba bado hawajui chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo.
Afisa mkuu mtendaji Edward Sirait ameambia shirika la habari la Reuters: "Hatuwezi kusema chochote kwa sasa. Tunajaribu kutafuta maelezo na data zaidi."
Vyombo vya habari Indonesia vimemnukuu afisa wa bandarini Tanjung Priok akisema kwamba maafisa wa boti la kusindikiza meli wameripoti kwamba wameviona vifusi vya ndege hiyo kwenye mai.
Suyadi, ambaye hutumia jina moja pekee kama raia wengi wa Indonesia, amesema vyombo vingine vya baharini vimefunga safari kuelekea eneo hilo.
Baada ya kusafiri kwa muda mfupi, ilitarajiwa kutua Pangkal Pinang saa moja baadaye.