Ndege za Jeshi zagongana, Uwanja Wafungwa
0
October 04, 2018
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum umefungwa baada ya ndege mbili za kijeshi kugongana leo.
Kwa mujibu wa Uongozi wa uwanja huo, ndege hizo aina ya Soviet-era Antonov zilitua kwa kuachiana sekunde chache na baadaye moja iligonga sehemu ya nyuma ya ndege nyingine.
Msemaji wa Uwanja huo, Mohamed Mahdi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hakuna watu waliopata madhara ya kuumia kutokana na ajali hiyo.
Aidha, Mahdi amesema kuwa Uongozi wa uwanja huo unaanzisha uchunguzi wa tukio hilo. Jeshi la Sudan halijatoa tamko lolote kuhusu ajali hiyo.
Hata hivyo, AFP imeripoti kuwa chanzo chake cha kuaminika kimesema watu nane walijeruhiwa na walipelekwa hospitalini.
Ajali hiyo ya leo ni ya tatu kuzikumba ndege za jeshi la nchi hiyo.
Septemba 21, marubani wawili wa ndege ya jeshi walikufa baada ya ndege yao kuanguka katika eneo la Omdurman. Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya chopa ya jeshi kuanguka ilipokuwa inatua katika uwanja wa jiji la Darfur; abiria wote waliokolewa huku chopa hiyo ikishika moto.
Tags