NECTA Yaitangaza Shule Nyingine Kinara Wizi wa Matokeo Darasa la Saba Mwaka Huu



Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limekitaja kituo kilichokuwa kitovu ya mtandao wa wizi wa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.

Oktoba 2, 2018  Necta ilitaja orodha ya shule zilizofanya udanganyifu na kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba uliofanyika Septemba 5 na 6, 2018.

Ilifuta matokeo ya shule zote za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, Shule ya Kondoa Integrity (Kondoa, Dodoma), Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy (Dar es Salaam), Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza.

Oktoba 9, Necta ilizitaja shule nyingine zilizoongezeka katika mtandao huo wa wizi kuwa ni Atlas (Ubungo), Atlas (Madale) na Great Vision zote za Dar es Salam.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 23, 2018 wakati akitangaza matokeo ya darasa la saba, Katibu mtendaji wa baraza hilo, Dk Charles Msonde amesema wizi huo ulifanyika katika kituo cha Nyanduga kilichopo halmashauri ya Lorya mkoani Mara.

"Uchunguzi umekamilika na baraza limejidhihirisha kuwa wamiliki wa shule na walimu wao walishirikiana kupata mitihani kwenye kituo teule cha shule ya msingi Nyanduga,” amesema.

Amesema baada ya kupata mitihani waliisambaza kwenye  shule nyingine ikiwamo  Hazina, New Hazina,  Alliance na New Alliance zilizopo halmashauri ya Mwanza ambazo zote zilifutiwa matokeo.

"Walitumia viongozi wa elimu wa ngazi mbalimbali katika halmashauri ya Lorya ili wizi huu uweze kufanikiwa," amesema.

Amewataja baadhi yao kuwa ni maofisa elimu, wasimamizi wa mitihani pamoja na walinzi. Amesema baadhi ya maofisa walifanya udanganyifu kwa kuchukua mitihani saa saba usiku.

"Kulikuwa na Marwa Mtatiro ambaye alikuwa mkuu wa Shule ya Nyanduga  pamoja na mwalimu Emma Macha aliyekuwa msimamizi mkuu wa kituo," amesema.

Amesema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wahusika kutokana na kuvunja viapo vyao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad