BAADA ya kudaiwa kuonyesha kiwango cha chini katika mechi ya ugenini dhidi ya Guinea, nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Haruna Niyonzima, amesema kuwa hafikirii kustaafu kuichezea timu hiyo.
nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Haruna Niyonzima picha na mtandao
Niyonzima alisema hayo kutokana na kushambuliwa kwa maneno na mashabiki wa Rwanda baada ya kufungwa mabao 2-0 na Guinea mjini Conakry ambao walimtaka kiungo huyo astaafu na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine chipukizi.
Hata hivyo, kiungo huyo hakupangwa katika mechi ya marudiano iliyochezwa Jumanne mjini Kigali na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
“Sina mpango wowote wa kustaafu kuichezea timu ya Taifa," alisema Niyonzima akijibu swali lililotokana na maoni ya wadau wa soka nchini humo.
Aliongeza kusema kuwa bado ana nafasi na muda zaidi wa kuitumikia Amavubi.
“Bado nina uwezo na muda wa kutosha kuichezea Amavubi. Baadhi ya watu wanataka nistaafu kuitumikia nchi yangu, lakini ninapenda kuwaambia kuwa bado nina uwezo wa kuitumikia Amavubi na klabu yangu, ” alisema kiungo huyo wa zamani wa Etincelles, Rayon Sports, APR za Rwanda na Yanga ya Tanzania.
Niyonzima kwa sasa amekosa nafasi ya kuwa kwenye kikosi cha kwanza katika klabu yake ya Simba ambayo inatetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, amekuwa nahodha wa Amavubi tangu Agosti mwaka 2013 akichukua mikoba iliyoachwa na Olivier Karekezi ambaye alistaafu kuitumikia timu hiyo.