Mbunge wa zamani wa jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amesema kuwa ni mapema sana kwa sasa kujua hatma yake ya kuwania nafasi yeyote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, akibainisha kuwa hivi sasa anapigania kupatikana kwa kwa tume huru ya uchaguzi.
Akizungumza na www.eatv.tv amesema hana msimamo juu ya kuwania nafasi yeyote ndani ya nchi licha ya baadhi ya wakosoaji wake wanaodai kuwa anajipanga kuwania nafasi ya urais kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Nyalandu amesema “malengo yangu ni kuona Tanzania inastawi kidemokrasia na inaruhusu upana wa mawazo na wale wanaoshinda watangazwe kwa pande zote mbili, hii itasaidia Tanzania na itasifika kidemokrasia, na nina matarajio tutafikia mahali nguvu ya nani awe kiongozi itakuwa ni maamuzi ya wananchi.”
“Sijasema nitatangaza au sitatangaza nia, ila tunaye rais mpaka kufikia 2020 tuendelee kumuheshimu ila lazima watambue kuna watu wengine ambao si wana CCM na wanahitaji fursa, lakini kwa sasa hivi tuangalie zaidi kwenye kujenga chama, sio muda wa kusema nani anakuwa kiongozi." Ameongeza Nyalandu
Nyalandu ni Mbunge pekee kutoka Chama Cha Mapnduzi (CCM) ambaye alitangaza kujivua nafasi yake na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai ya kukosekana kwa Demokrasia ndani ya chama chake cha zamani.