Rais Magufuli amesema, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, Julius Nyerere kwa kuhakiksha fikra na mipango mizuri aliyoiweka inatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.
Amesema, Baba wa Taifa alifanya kazi kubwa kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano na pia kujenga misingi ya uchumi wa kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
Akiwa nyumbani kwa Mjane wa Baba wa Taifa, Rais Magufuli pia alikutana na mtoto wa Mwl. Nyerere, Makongoro na wajukuu wa Baba wa Taifa.
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hiyo ndiyo iliyompatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la “Mwalimu.” Kwanza aliongoza Tanganyika toka mwaka 1961 hadi 1964 kama waziri mkuu, halafu kama rais; baada ya muungano wake na Zanzibar, aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985 kama rais.
Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda mrefu, akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi. Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Hata hivyo aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Related Articles