Ombaomba aliyenasa siku za nyuma alikuwa akifanya shughuli zake hizo ambazo siyo halali katika eneo la Posta mjini hapa na wananchi wamesema ameibuka mwingine ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja. Walisema ombaomba huyo amekuwa na tabia ya kuomba chochote na unapokataa hutoa kisu kukutisha.
“Mimi niliwahi kukimbizwa na ombaomba huyo ambaye huja mara kwa mara maeneo hayahaya ya Posta hapa mjini kama alivyokuwa akifanya yule aliyekamatwa na Polisi, ” alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Monica John mkazi wa Frelimo.
Mama huyo alisema alikumbana na ombaomba huyo eneo hilo na alipomwambia hana kitu alimtolea kisu naye akakimbia kuokoa roho yake. Mama huyo aliongeza kuwa anavyoona yeye kijana huyo hana matatizo ya akili kwa sababu amekuwa akichagua wanawake tu anapotaka fedha.
Monica aliongeza kuwa aliambiwa na watu kwamba ombaomba huyo huwafuata wanawake kwa kuwa ni rahisi kwao kumpa fedha wakitishwa na ni nadra kumuona akiwaomba wanaume. “Bila shaka anajua kwamba akimtishia mwanaume anaweza kupewa mkong’oto ndio maana anaonea wanawake wanaopita eneo hilo la Posta,” alisema mama huyo.
Mwana mama mwingine Fidea James, mkazi wa Mshindo alisema kuwa kwa kuwa ni siku moja moja kijana huyo anafanya kitendo hicho ni vema polisi wakafanya doria eneo hilo ili waweze kumnyaka kama walivyomnasa mwingine siku za nyuma.
“Huko nyuma kuliwahi kutokea ombaomba mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Mohamed ambaye naye alikuwa akitumia kisu kutishia mtu ambaye alikuwa akimuomba fedha na kukataa kumpa,” alisema Fidea.Akaongeza:“Huyo Mohamed alikuwa mtu mtanashati tu, lakini alikuwa na tabia hiyo ya kuomba fedha na usipompa alikuwa akitishia kwa kuchomoa kisu,” alisema mama huyo. Alisema kwa kuwa za mwizi huowa ni 40, kijana huyo siku moja alitishia kumchoma mtu kisu mbele ya askari polisi na akakamatwa na kutiwa ndani na hadi leo hawajamuona baada ya polisi kufanya kazi yako nzuri.
Kipindi hicho Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Peter Kakamba alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na akawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi wanapoona watu kama hao kwani alisema ni hatari kwa jamii. Mwananchi mwingine, Abdallah Hussein alisema wananchi wanatakiwa kuna na tahadhari, hasa nyakati za jioni kwani kijana huyo huvizia anapoona hakuna pilikapilika za watu kupita mitaani.