Mbunge wa Babati Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Manyara na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Kanda ya Kaskazini Pauline Gekul amejivua uanachama wa Chadema, na kujiuzulu nafasi zote za uongozi alizokuwa nazo usiku huu na kujiunga na chama cha mapinduzi (CCM).
Gekul ametaja sababu mbili za kufanya maamuzi hayo. Ya kwanza ni chama kuwabebesha wabunge mzigo shughuli za ujenzi wa chama.
Gekul ameendelea kusema kuwa kwenye chaguzi ndogo zote zilizofanyika Manyara alitoa fedha zake mfukoni kugharamia, na chama kilileta laki tano tu, licha ya kwamba kinapokea ruzuku ya zaidi ya milioni 300 kwa mwezi. Pili amesema ni kupigwa majungu na viongozi wenzie wa Chadema.
Mheshimiwa Gekul anakuwa mbunge wa nane wa upinzani na tisa wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muunganobwa Tanzania chini ya Spika Ndugai kujiuzulu.
Katika wimbi hili la hama hama ya wabunge hadi sasa ni Lazaro Nyalandu pekee aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM alijiuzulu na kujiunga na Chadema.
Hadi sasa wabunge wa upinzani waliojiuzulu na kutimukiia CCM walikopitishwa na kugombea na sasa ni wabunge ni Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) na Dk Godwin Mollel (Siha-Chadema).
Wanaosubiri kuapishwa ni; Mwita Waitara (Ukonga-Chadema) na Julius Kalanga (Monduli-Chadema) huku Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF) huenda akaibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi Oktoba 13,2018.
Wengine waliojizuli hivi karibuni ni; Mwarya Chacha (Serengeti-Chadema) na James Milly wa Simanjiro naye Chadema.