Raia Wawili Wa China Watimuliwa Nchini Kwa Kosa la Kuwatwanga Ngumi Watanzania


Serikali  imewatimua nchini raia wawili wa China kwa kosa la kuwatwanga makonde na kuwanyanyasa Watanzania walioajiriwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya Makongorosi mkoani Mbeya, inayojengwa kwa kiwango cha lami.


Uamuzi wa kuwafukuza Wachina hao ulitolewa juzi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye mradi huo, unaotekelezwa na Kampuni ya China Railway 15 Beaural Group Corporation Ltd.


Wakati akiendelea kukagua mradi huo, Waziri Kamwelwe alisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Matundasi, ambao walimweleza manyanyaso wanayoyapata, ikiwamo kupigwa, na wasimamizi wa mradi huo, raia wa China.


Mmoja wa wananchi hao ambaye ni wafanyakazi kwenye kampuni hiyo, Wilson Pawa, alisema makandarasi hao wanawanyanyasa kwa kuwasingizia kuwa wanawaingizia hasara na ikitokea wakabishana huanza kuwapiga kung-fu na kutishia kuwaua kwa risasi.


"Hawa Wachina ukimaliza kazi wanasema umewatia hasara. ukibisha wanaanza kutupiga kung-fuu na wanatutishia kutuua na wanatupiga kweli kweli si mchezo. Mimi hadi sasa nina uvimbe na maumivu makali na nimechukua PF 3 (fomu ya matibabu kutoka polisi) kwa ajili ya matibabu," alisema Pawa.


Naye Mapuli Mbumba, ambaye ameajiriwa na kampuni hiyo katika nafasi ya dereva, alisema Wachina hao wanaajiri bila kuwapatia mikataba ya ajira na kila ikifika mwisho wa mwezi, wanakata mishahara yao bila sababu za msingi kinyume cha makubaliano.


Alisema kutokana na unyanyasaji huo, wananchi hawana uhusiano mzuri na kampuni hiyo, jambo ambalo linahatarisha amani miongoni mwao.


"Tunajua sheria inataka wakituajiri watupatie mikataba ya ajira, lakini wenzetu hawa hawatoi mikataba na mwisho wa mwezi wanatukata mishahara na wakiamua wanakufukuza wanavyotaka. Kwa kweli wanatunyanyasa sana," alisema Mbuba.


Diwani wa Matundasi, Kimo Choga, alisema mbali na kero hizo, pia kuna tatizo upande wa magari yanayotumiwa na Wachina hao kujenga barabara kuwa ni mabovu na yanaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.


Alisema magari hayo hayana taa, vioo vya kutazamia nyuma (site mirror) na taa za ishara (indicator), hali ambayo kama yakiongozana na gari lingine dereva hawezi kujua kama limesimama, hivyo ni rahisi kusababisha ajali.


Choga pia alidai kuwa makandarasi hao hawajali hata kumwaga maji kwenye barabara zinazojengwa na zile zinazotumika wakati wa ujenzi hali ambayo inasababisha makazi ya watu kujaa vumbi na kuhatarisha afya za wananchi.


Waziri Kamwelwe pia alihoji utendaji kazi wa Wachina hao katika utekelezaji wa mradi huo, ndipo Mwakilishi wa Kampuni ya SMEC Company Ltd inayosimamia mradi huo kwa niaba ya serikali, Gosbert Luburi, aliposema hadi sasa utekelezaji uko nyuma ikilinganishwa na ratiba ya mkataba.


Alisema hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo umetekelezwa kwa asilimia 13 wakati kwa mujibu wa ratiba ya mkataba, ulipaswa kuwa umekamilika kwa asilimia 20.


Luburi alimweleza Waziri Kamwelwe kuwa kandarasi huyo aliahidi kuwa hadi Januari, mwaka huu, angekuwa ameleta wataalam saba kushugulikia mradi huo lakini hadi sasa wataalam waliopo ni watatu tu.


"Mkandarasi huyu aliahidi kuwa angeleta mitambo 74 kufikia Januari, mwaka huu, lakini hadi sasa mitambo iliyopo ni 34 hali ambayo inasababisha kazi hii kutofanyika kama ilivyopangwa," alisema Luburi.


Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Waziri Kamwelwe alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia unyanyasaji wa aina hiyo wa kuwapiga wananchi na aliufananisha unyanyasaji huo na ukoloni hivyo akatoa uamuzi wa kuwatimua nchini wasimamizi wawili wa mradi huo waliotajwa na wananchi kuhusika na unyanyasaji ikiwamo kuwashushia kipigo.


Alisema barabara hiyo inajengwa kwa kodi za Watanzania kwa asilimia 100 na kwamba kwa mantiki hiyo Watanzania wa chini ndio waliowaajiri Wachina hao kupitia kodi zao, hivyo hawatakiwi kupata manyanyaso yoyote.


"Ndugu wananchi najua mnayo mambo mengi lakini mimi nachukua uamuzi ufuatao. Kuanzia sasa, naamuru Wachina hawa wawili waondoke warudi kwao China. Sitaki tena kuwaona hapa nchini. Naagiza Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) kuwa watu hawa waondoke," alisema Kamwelwe.


Aidha, Waziri Kamwelwe aliagiza kufutwa mara moja kwa vibali vya watu hao kufanya kazi nchini na kuamuru Tanroads kutekeleza agizo hilo mara moja.


Waziri Kamwelwe pia alitoa miezi mitatu kuanzia sasa hadi mwezi Januari, mwakani, kampuni hiyo kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika katika ujenzi wa barabara hiyo vinafikishwa eneo la mradi na wataalamu wote wanaohitajika huku akiwataka kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyomo kwenye mkataba.


"Nitarudi hapa Januari na ninataka nikute maagizo yangu yametekelezwa, vinginevyo nitavunja mkataba huu na kumpatia mtu mwingine atujengee barabara," alisema.


Barabara ya Chunya – Mangongorosi yenye urefu wa kilomita 39 inajengwa kwa kiwango cha lami na serikali ya Tanzania kwa lengo la kuunganisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na ile ya Kanda ya Ziwa kwa barabara ya lami.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad