Rais Mkapa alikuwa sahihi tumrudie'' - Lwaitama

Rais Mkapa alikuwa sahihi tumrudie'' - Lwaitama
Baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kuzifutia matokeo ya mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi, shule nane nchini, wadau wa elimu wameomba hoja ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ya kuwepo kwa mjadala wa elimu wa kitaifa ipewe kipaumbele.

Akiongea leo kwenye MJADALA kupitia East Africa Television, Mhadhiri mwandamizi mstaafu na mchambuzi wa masuala ya elimu, Azavel Lwaitama amesema kuna haja ya kurejea nyuma na kuifanyia kazi hoja ya Rais Mkapa ya kuwepo kwa mjadala wa kitaifa juu ya elimu yetu.

''Mifumo ya elimu yetu ina shida kuanzia elimu ya msingi maana ukitaka kuona kuna tatizo unashangaa mtu anafoji vipi mtihani wa darasa la saba ambao ni kuandika na kujibu hesabu tu kitu ambacho hakihitaji kufikiria sana na hapa ndipo umuhimu wa hoja ya Rais Mkapa unakuja'' - amesema Lwaitala.

Aidha Mhadhiri huyo mstaafu ameshauri kuwa kuna haja ya kushirikishwa kwa wabobezi wa elimu watazame mifumo kisha waje na njia nzuri ya nini kifanyike kuinua elimu yetu ili kuepuka ushindani mbaya wa kufoji na badala yake kuwepo na ushindani mzuri wa kufaulisha kwa taaluma halisi.

Oktoba 2, 2018, NECTA ilizifutia matokeo shule za Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fount of Joy za Dar es Salaam, Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza  na Kondoa Integrity ya Kondoa  kwa tuhuma za kuvujisha mtihani huo.

NECTA pia ilifuta matokeo ya mtihani huo kwa shule zote za msingi za halmashauri ya Chemba na kutangaza kurudiwa tena Oktoba 8 na 9 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad