Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (TLS), Fatma Karume amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kwa agizo alilotoa kwa Jeshi la Polisi, kutoa dhamana kwa watuhumiwa siku zote saba za wiki kwa masaa 24.
Karume ametoa kauli hiyo kwenye kipindi cha East Africa BreakFast kinachoruka East Africa Radio kuanzia saa 11 Alfajiri, ambapo amesema suala la Polisi kutoa dhamana Jumamosi na Jumapili ni wajibu wao, kama wanafanya kazi siku hizo na wanalipwa
Karume ameongeza kuwa Polisi wana wajibu wa kuwapa watu dhamana, na iwapo watalazimika kuendelea kumshikilia mtuhumiwa wanatakiwa kuongeza masaa 8, na iwapo itahitajika zaidi ni lazima wapate kibali cha mahakama.
Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (TLS), Fatma Karume.
"Polisi sio mahabusu, mahabusu ni jela na huwa pale mahakama imeamua kuwa wewe hustahili kupata dhamana, polisi hakuna mahabusu, polisi hawana haki ya kukuweka selo kwa zaidi ya saa 24", amesema Karume.
Karume mesisitiza kuwa, "Inawezekana huyu mtu ana watoto, anafanya kazi na anatakiwa kazini, iwapo utamshikilia mtu na umemnyima haki ya dhamana, akakaa bila kwenda kazini labda, ikamuathiri kufukuzwa kazi, ni umemnyima haki yake".
Septemba 30, Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, alitoa agizo kwa Jeshi la Polisi Nchini kuhakikisha dhamana kwa watuhumiwa inatolewa kwa saa 24 katika siku zote 7 za wiki, tofauti na zamani ambapo ilikuwa inatoka mwisho Ijumaa jioni.
Lugola alitoa agizo hilo wakati akiongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Basanza wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.