Na John Walter-Babati
Watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Manyara baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya Mirungi kilo tano sawa na mabunda 14 yakisafirishwa kutoka mkoani Arusha kwenda Babati.
Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara Agustino Senga amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Oktoba 6-2018 Majira ya saa 12 Jioni katika kituo cha ukaguzi wa magari eneo la Minjingu kata ya Nkaiti wilaya ya Babati wakiwa wameficha madawa hayo ya kulevya kwenye miili yao maeneo ya tumboni hadi mgongoni.
Amewataja waliokamatwa ni Aisha Mohamedi [38] mkazi wa Endasaki, Amani Hassan [30] mkazi wa Sakina Arusha ambao walikuwa wakisafirisha Mirungi kilo hiyo iliyokuwa imefungwa kwenye magazeti na kuwekwa gundi ya karatasi na kisha kuifunika kwenye nguo walizokuwa wamevaa.
Senga amesema Watu hao walikamatwa wakiwa katika gari kampuni ya Makara yenye namba za Usajili T 128 -PDC Fuso wakiwa wamejifunga madawa hayo kwa mabunda madogo madogo 14 wakiwa wamejizungushia tumboni ili kuonekane ni mtu mwenye vitambi au mwenye ujauzito na muda wowote watapandishwa kizimbani.
Ikumbukwe kwamba Matumizi ya madawa ya kulevya yameathiri vijana wengi kiafya kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya kazi , hivyo kulazimika kujihusisha na matukio ya wizi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kamanda amewatahadharisha wakazi wa mkoa wa Manyara na wanaoingia katika mkoa huo kwamba Mkoa wake sio mlango wa kupitisha madawa ya kulevya.
RPC Manyara Agundua Mbinu Mpya Za Kusafirisha Madawa Ya Kulevya
0
October 09, 2018
Tags