UTAFITI umebaini kuwa wananchi wa Rwanda wataendelea kuongoza katika kuishi miaka mingi katika nchi za Afrika Mashariki mpaka 2040 na kufuatiwa na wananchi wa Kenya.
Mabadiliko hayo yanatokana na aina ya vyakula na mazingira wanayoishi. Kwa sasa Rwanda ina wastani wa uwezo wa kuishi akiwa miaka 67.8, ikikua kufikia miaka 74.8 na hali ikiendelea vema itafikia miaka 77.6 kwa mazingira bora ya afya.
Kenya ikishika nafasi ya pili katika nchi za ukanda huo ikiwa na wastani wa wananchi wake kuishi miaka 66.9 huku ikitarajiwa mwaka 2040 itaongezeka kwa miaka 73.9 na ikiwa serikali itaboresha huduma za afya itakua kwa miaka 78, hivyo kuchukua nafasi ya Rwanda.
Akitangaza jijini Washington, Marekani juu ya utafiti mpya uliochapishwa na gazeti la Tiba la Kimataifa la The Lancet, Mkurugenzi wa Takwimu katika Taasisi ya Afya na tafiti, Dk Kyle Foreman, alisema Tanzania wastani wa umri wa kuishi kwa sasa ni miaka 64.3 huku ikitarajiwa kufikia miaka 72.3 kwa mikakati ya sasa na ikiboreshwa zaidi itafikia miaka 75.9.
Kwa sasa Uganda ina wastani wa umri wa kuishi wa miaka 62.2 na ikitarajiwa kuongezeka kufikia umri wa miaka 69.5 mwaka 2040, huku mwaka 2040 ikitarajiwa kuongezeka mpaka miaka 72.8 ikiwa huduma za afya zitaboreshwa.
Utafiti umeonesha kuwa changamoto kubwa ya umri wa kuishi ni magonjwa yasiyoambukizwa yanayotarajiwa kuwa sababu kubwa ya vifo vya watu katika nchi za Afrika Mashariki ifikapo 2040, yakiwemo kisukari, figo, saratani za aina mbalimbali na uzito uliokithiri.