Safari ya Hawa India Kutibiwa Figo Yaiva...Uongozi wa Diamond Wafunguka


Uongozi wa lebo ya Wasafi, umebainisha kuwa safari ya Hawa Said ‘Hawa Nitarejea’ kwenda kupata matibabu nchini India imeiva na kueleza siku ambayo atasafiri.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumamosi Oktoba 6, 2018 meneja wa Diamond, Babu Tale amesema walikuwa wakihangaikia viza kwa ajili ya kumpeleka nchini India na wanatarajia kuondoka nchini Jumatano ijayo.

Diamond jana alipokuwa uwanja wa Magunia katika mfululizo wa kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa kadi za bima ya afya, mitaji na zawadi mbalimbali kwa wakazi wa Tandale alizungumzia safari ya Hawa.

Amesema katika safari hiyo, Hawa anatarajiwa kutumia si chini ya Sh11 milioni kwa ajili ya kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake.

“Niliamua kukaa kimya kuhusu suala la kumsaidia Hawa lakini kwa bahati mbaya sana watu walikuwa wakiyaongea kwenye mitandao mambo wasiyoyajua mpaka pale nilipoamua kuweka hadharani,” amesema.

“Hata hivyo baada ya kubainika kwamba Hawa ugonjwa wake unatakiwa matibabu zaidi nje ya nchi, nimeamua kumsaidia kama binadamu na kwa uchunguzi tu wa ugonjwa wake, atatutumia sio chini ya Sh11 milioni.”

Akizungumzia hatua hiyo, Hawa amesema alichokifanya Diamond kwake ni kama sadaka na kuwaomba Watanzania wamuombee akatibiwe, apone na kurejea nyumbani salama.

“Bado ninaumwa, kwa sasa siwezi kusema lolote kwani silali vizuri, siwezi kula vizuri yaani kwa ufupi ninaumwa na sina raha, ngojeni niende kwenye matibabu nikirudi salama basi nitakuwa na la kuongea zaidi kwa alichokifanya Diamond kwangu,” amesema Hawa.

Kwa upande wake mama wa Hawa,  Ndagina Shabani amesema katika safari hiyo anatarajia kusafiri na mgonjwa japokuwa hakutaka kuweka wazi zaidi kama wameshapatiwa tiketi za kusafiri hadi sasa.

Hawa Said maarufu kwa jina la ‘Hawa Nitarejea’ anasumbuliwa na ugonjwa wa kujaa maji tumboni uliosababishwa na tatizo katika ini.

Kutokana na ugonjwa huo amewahi kulazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad