Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam jana usiku Oktoba 21, 2018 lilimhoji kwa saa kadhaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kuhusiana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amethibitisha mahojiano hayo na kwamba waziri huyo aliruhusiwa kuondoka baada ya kuhojiwa.
Mo Dewji alitekwa Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi na kupatikana Oktoba 20 saa nane usiku, baada ya waliomteka kumtelekeza katika viwanja vya Gymkhana, jijini Dar es Salaam.
Makamba ni miongoni mwa watu waliopata taarifa mapema za kupatikana kwa bilionea huyo na kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Katika ukurasa wa Twitter Makamba aliandika, “Mohammed Dewji amerudi nyumbani salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 30 zilizopita. Sauti yake inaonyesha mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”