Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Simba, Adam Salamba ameweka wazi sababu ya kushangilia kwa ishara ya kupiga gitaa baada ya kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi kuu soka Tanzania bara akiwa na klabu ya Simba.
Salamba ambaye alifunga bao hilo usiku wa Jumatano kwenye ushindi wa mabao 5-1, ambao Simba iliupata dhidi ya Alliance FC kwenye uwanja wa taifa, amesema kwasasa anajifunza gitaa hivyo alikuwa anatuma ujumbe kwa mwalimu wake wa gitaa.
"Nilishangilia kama napiga gitaa ili kum'support' rafiki yangu Max ambaye amekuwa akinifunza kutumia gitaa. Mara nyingi nikitoka kwangu naenda kwake kujifunza hivyo nilimuahidi siku nikifunga nitashangilia kwa namna ile."
Hata hivyo Salamba ambaye siku hiyo alikuwa anaanza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwenye mchezo wa ligi kuu tangu ajiunge nayo mwezi Julai akitokea Lipuli FC, amesema anashukuru kwa kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi akiwa na Simba.
''Ni hatua nyingine kwenye maisha yangu ya soka na nina furaha nimeweza kuifungia timu yangu na nitaendelea kujituma kila ninapopata nafasi ya kucheza'', ameongeza.
Katika mchezo huo Salamba alifunga bao la 4 kwa kichwa na kukimbilia kwenye kibendera cha eneo la kona ambapo alikishika na kuonesha ishara ya kupiga gitaa.