Saudi Arabia Yakiri Kumuua Jamal Khashoggi

Saudi Arabia Yakiri Kumuua  Jamal KhashoggiMwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliuawa katika vita katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, runinga ya taifa hilo imesema ikinukuu uchunguzi wa awali.

Naibu afisa mkuu wa idara ya Ujasusi Ahmad al-Assiri na mshauri mkuu wa Mwanamfalme Mohammed Bin Salma Saud al-Qahtani walifutwa kazi kufuatia kisa hicho.

Wakati huohuo huo Uturuki imeapa kufichua maelezo yote kuhusu mauaji ya mwandishi huyo , baada ya Saudia kukiri kwa mara ya kwanza kwamba aliuawa katika ubalozi wake mdogo mjini Istanbul.

'Uturuki haitaruhusu mauaji yake kufichwa', alisema msemaji wa chama tawala cha taifa hilo.

Saudia ilisema siku ya Ijumaa kwamba Bwana Khashoggi , ambaye ni mkosoaji maarufu wa Saudia alifariki alipokuwa 'akipigana ngumi'.

Maafisa wa Uturuki awali walikuwa wamesema kuwa aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwa katwa.

Mapema wiki hii maafisa wa Uturuki ambao hawakutaka kutajwa waliambia vyombo vya habari kwamba walikuwa na ushahidi wa sauti na kanda za video kuthibitisha hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa kile kilichotokea hakitakubalika lakini akaongezea kuwa Saudia ni mwandani wake mkuu.

Hii ni mara ya kwanza kwa ufalme huo kukiri kwamba Khashoggi amefariki. Saudia imesema kuwa haikushiriki katika kutoweka kwa mkosoaji wake mkubwa wakati alipoingia katika ubalozi mdogo mjini Istanbull tarehe 2 Oktoba ili kutafuta vyeti vya harusi yake.

Ufalme wa Saudia ulikuwa umeshinikizwa kuzungumza kuhusu kutoweka kwa bwana Khashoggi baada ya maafisa wa Uturuki kusema kuwa aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwakatwa.

Siku ya Ijumaa maafisa wa polisi wa Uturuki waliendeleza upekuzi wao hadi katika msitu mmoja jirani ambapo maafisa wasiotaka kujulikana wanaamini mwili wake ulikuwa umetupwa.

Wachunguzi wanahoji iwapo washirika wa Saudia kutoka mataifa ya magharibi wataamini madai hayo ya Saudia na iwapo itawashawishi kutochukua hatua zozote kali dhidi ya taifa hilo.

Wizara ya maswala ya kigeni nchini Uingereza imesema kuwa inafikiria kuchukua hatua baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad