Mbunge wa Jimbo la Siha, Dkt Godwin Mollel amesema hana ugomvi na Mwenyekiti wa Chama chake cha zamani Freeman Mbowe licha ya kuwepo kwa baadhi ya wabunge ndani ya CHADEMA ambao anadai kutoelewana nao kwasababu ya maamuzi yake ya kukihama chama hicho.
Kauli hiyo ya Dkt Mollel imekuja siku chache baada ya kudai kuwa hajawahi kuingia kwenye vita ya kitoto, hali ambayo ilionesha baada ya kufanya maamuzi yake kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilimuingiza kwenye mgogoro na baadhi ya waliokuwa wabunge wa upinzani.
Akizungumza na www.eatv.tv Dkt Mollel amesema “sina tofauti na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, Mbowe hana shida ni mwenzetu ni rafiki yetu, na niliposema tuna vita sio vita ya ugomvi ni vita ya kisiasa hasa kwenye ubishi wetu wa sera ipi ambayo nzuri kuifuata.”
“Wakati naondoka sikugombana na Mbowe na mtu yeyote ila nimegombana na namna wanavyofikiri kuhusu nchi yetu ndio maana nikaona bora nifuate fikra za Rais Magufuli ndio zilizokuwa sahihi”, ameongeza Dkt Godwin Mollel.
Hivi karibuni, Dkt Mollel alinukuliwa akisema “sitakaa nijutie kuhama CHADEMA, ndio maana nimeungwa mkono na niliwaambia watu huwa siingii vita ya kitoto, na sijaingia vita ya kitoto, pia nimesikia wataondoka wabunge karibia wote na watabaki kumi, na wakati wa uchaguzi atashinda mbunge mmoja ambaye kwa sasa siwezi kumtaja.”