HILI ni pigo kwa waigizaji! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kampuni maarufu ambayo mastaa wa filamu walikuwa wakifanya nayo kazi, Steps Entertainment kufunga ofisi, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.
Chanzo makini kililipenyezea habari gazeti hili kuwa kwa muda mrefu sasa kampuni hiyo imefunga ofisi ya filamu kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji kwani soko la filamu limeshuka na biashara hakuna tena.
“Steps wameamua kuachana na mambo ya kuchezesha mastaa filamu na kusambaza kwa sababu hali ya soko ni mbaya na wanatakiwa kulipa kodi, sasa wakaona hakuna faidi ndiyo wameamua kuachana nayo na sasa wanashughulika na biashara nyingine.
“Kwa sasa hali ya maisha itazidi kuwa mbaya sana kwa mastaa wa filamu ambao walikuwa wakitegemea kazi hiyo tu na hawakujiongeza mapema kwa kufanya hata biashara kwani kampuni hiyo ilikuwa ndiyo tegemeo kubwa kwao katika kuwasambazia filamu na kuwapa mikataba ya kufanya nao kazi,” kilisema chanzo.
Image result for Steps Entertainment
Baada ya kupata taarifa hizo, Risasi Mchanganyiko lilifika katika ofisi hizo zilizopo Kariakoo, Dar na kushuhudia zikiwa zimefungwa huku baadhi ya sehemu ya ofisi hiyo vyumba vingine vikigeuzwa maduka ya kuuza vifaa mbalimbali na vingine wakiwa wanauza nyimbo na tamthiliya kwenye flash.
Katika jitihada za kuwatafuta wahusika ili waelezee ukweli juu ya habari za kufunga ofisi hiyo, gazeti hili lilifanikiwa kupata mawasiliano ya msemaji wa kampuni hiyo ambaye alikiri kwamba ni kweli. Akizungumza kwa njia ya simu, msemaji wa Steps aliyejitambulisha kwa jina moja la Carlos alieleza kuwa wameamua kufunga ofisi hiyo kwa muda kwa sababu maharamia wamekuwa wengi hivyo kusababisha soko kuwa gumu.
“Tumefunga ofisi kwanza kwa muda kuangalia soko kwanza. Soko limekuwa gumu sana kutokana na maharamia kuwa wengi hivyo hali hiyo ikibadilika na kuwa nzuri tutarejea,” alisema Carlos. Kampuni ya Steps ilikuwa ni kampuni kubwa ya kusambaza filamu ambapo ilikuwa ikifanya kazi na mastaa mbalimbali akiwemo Jacob Steven ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Hisan Muya ‘Tino’ na wengine wengi.