Taharuki Yatanda Kagera Baada ya Mwanamke Kujifungua mfuko wa rambo wenye takataka

Taharuki Yatanda Kagera Baada ya Mwanamke Kujifungua mfuko wa rambo wenye takataka
Sara Daniel (22), mkazi wa kijiji cha Bulego, Ngara mkoani Kagera, amezua taharuki kwa wananchi, baada ya kujifungua mfuko wa rambo wenye takataka.

Tukio hilo la aina yake limemkuta mwanamke huyo mara nne mfululizo katika kipindi cha mwezi huu, licha ya ujauzito alioubeba wa miezi minane sasa.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 12, mwaka huu, nyumbani kwao katika kitongoji cha Kigona, mara baada ya mwanamke huyo kusikia uchungu na kujifungua.

Akisimulia mkasa huo, mume wa mwanamke huyo, Josia Philemon, alisema kabla ya siku ya tukio hilo Oktoba 5, mwaka huu, mke wake alilalamika kusikia uchungu.

Philemon alisema baada ya hapo, alijifungua mfuko wa rambo wenye taka na siku mbili zilizofuata, hali hiyo ilijirudia tena kwa kujifungua mifuko yenye taka, hali iliyowalazimu kumpeleka hospitalini.

"Aliamka siku ya Jumapili tena akadai anasikia vichomi sana tumboni. Wakati tunasema tujiande kwenda hospitalini, alianza kusikia maumivu kama ya uchungu na muda mfupi baadaye, alijifungua mfuko huo wa rambo mweusi," alisema.

Philemon alisema baada ya kujifungua mfuko wa rambo kwa mara ya tatu, waliuchana ili wajue ndani yake kuna nini ndipo walipokuta mkaa, vibao, mawe, msumari, jivu na majani ya mgomba.

"Baada ya kuona vitu hivyo tuliamua kumpeleka hospitalini ambako daktari alihitaji kuviona, tukarudi kuchukua tukampelekea akaona," alisema.

Pia alisema baada ya daktari kumfanyia vipimo walibaini kuwa mimba yake ipo na ilikuwa ikiendelea vizuri.

"Walimlaza kwa siku tatu ili kuangalia hali yake inaendeleaje na walipoona anaendelea vizuri walimruhusu kurudi nyumbani," alisema Philemon.

Kwa mujibu wa mume huyo, baada ya kurudi nyumbani Oktoba 12, mwaka huu, tukio hilo lilijirudia na mke wake alijifungua tena mfuko mweusi wa rambo wenye takataka.

Alitaja vitu walivyokuta ndani kuwa ni karatasi iliyoandikwa kuwa 'mchawi ameshindwa', msumbari wa inchi tatu, noti ya fedha ya zamani iliyoandikwa East Afrika (Afrika Mashariki) ambayo pia imetobolewa.

Alisema vitu vingine vilivyokutwa ni miti miwili iliyofungwa kwa kamba za maji, vigae vya chungu, mikaa, chumvi na majivu.

Philemon alisema ndoa yao ina miaka mitatu na tayari wana mtoto mmoja na mimba ya pili ya mke wake iliharibika kabla ya kubeba hiyo ya tatu yenye mauza uza.

Alisema anampenda sana mke wake na hayuko tayari kumuacha kwa sababu za mauza uza hayo na kumtaka anayehusika na tukio hilo awasamehe kwa kuwa hakumbuki kama kuna kitu kibaya aliwahi kumfanyia mtu.

"Naomba kama kuna mtu nimemkosea kwa namna yoyote ile anisamehe. Najua hakuna mtu anayenidai na kama ananidai mimi sijui, aje aniambie tu nimlipe hata kama sina hela, nipo tayari kwenda kumlimia shamba lake, kuliko kuendelea kumtesa mke wangu hivi," alisema Philemon.

Kwa upande wake, Sara alisema tangu amebeba ujauzito huo, amekuwa akipatwa na mauzauza ambayo haelewi chanzo chake.

Alisema amekuwa akisikia maumivu ya tumbo yanayoambatana na uchungu na baadae kujifungua.

"Nimekuwa nikisikia dalili za uchungu mara kwa mara na nguvu zikiniishia na nikijifungua nazaa mfuko wa rambo wenye takataka,"alisema Sara.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Murugwanza, Lemi Andrew, ambako alipelekwa mama hiyo, alisema baada ya kumpokea alimpima na kubaini bado ana ujauzito wa miezi nane na kwamba hana tatizo lolote la kuuhatarisha.

Alisema walimpa ushauri na kumruhusu arudi nyumbani na endelee na ratiba zake za kwenda kliniki na inapotokea amepata tatizo lolote aende hospitali iliyokaribu.

Mganga huyo alitaja vitu alivyovishuhudia kuwa ni majani ya mgomba, makasha ya konokono, mawe na waya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad