PAMOJA na kwamba ilizidiwa ujanja na Cape Verde na kuchapwa mabao 3-0, moja ya kitu kilichoiangusha Taifa Stars ni kuwadharau wapinzani.
Abdi Banda, mmoja wa wachezaji wa timu hiyo amebainisha kuwa moja ya sababu ni kwenda na matokeo kichwani kuwa Cape Verde ni timu ya kawaida sana na si kama Uganda ambayo siku kadhaa zilizopita waliilazimisha sare ya bila kufungana nyumbani kwao.
Hii ni tabia ambayo imeota mizizi sana kwenye soka la Tanzania kuanzia kwa mashabiki na sasa imehamia kwa wachezaji.
Hata ukiangalia matokeo ya mechi za Stars utagundua kuwa inaponzwa mno na kutoziheshimu timu za nchi ambazo hazina majina makubwa kwenye soka la Afrika.
Stars hutumia nguvu nyingi na wachezaji kujituma zaidi inapocheza na nchi ambazo ziko juu kisoka kama Burkina Faso, Cameroon, Nigeria, Afrika Kusini, Misri na nyinginezo.
Lakini inapofika kucheza na timu za nchi ambazo majina yao si makubwa sana kwenye soka, basi wachezaji wanaonekana kama wanadharau mechi, lakini pia hata mashabiki wanajipa matumaini makubwa kana kwamba Tanzania iko juu mno kisoka kama zile nchi za Afrika Magharibi.
Kwa wenzetu wa Afrika Magharibi na Kaskazini hutumia mechi dhidi ya timu zisizo na majina kusaka ushindi kwa nguvu yoyote ile na itakapocheza na timu ambazo zinafanana basi hata sare inawatosha.
Huenda Banda atakuwa karibu na ukweli, kwani Stars iliyocheza dhidi ya Uganda ni ile ile iliyocheza dhidi ya Cape Verde, lakini wachezaji hawakucheza kama mechi ile ya kwanza.
Ukiangalia hata matokeo ya mwanzo, Stars iliyotoka sare dhidi ya Lesotho kwa bao 1-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex mwaka jana, inawezekana kabisa ilitokana na dharau kwa nchi ambazo hazina majina makubwa kwenye soka. Ni mechi ambayo Stars ilitakiwa kushinda ikiwa nyumbani endapo ingecheza kama ilivyopambana na Uganda.
Ukweli ni kwamba kwa sasa soka duniani limebadilika sana, hivyo wakati tunadhani Cape Verde au Lesotho zipo kama tunavyodhani sisi, inakuwa sivyo.
Ndiyo maana tuliona nchi kama Iceland ilifanikiwa kutinga fainali za Kombe la Dunia, huku nchi kama Italia ikizikosa. Juzi tu imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mabingwa wa Kombe la Dunia, Ufaransa, tena mabingwa hao walikuwa nusura walale, lakini uzoefu ukawasaidia kutoka nyuma ya mabao 2-0 hadi kusawazisha yote kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa.
Nchi kama Croatia si wengi waliotegemea kama ingeweza kutinga hatua ya robo fainali, achilia mbali fainali, lakini ikafanya hivyo na kuwaacha wengi midomo wazi. Hili ndilo soka ambalo Watanzania inabidi tujifunze.
Hata kundi lilivyopangwa, mashabiki wengi walifurahia na kuona kama Stars inaweza kwenda Afcon kirahisi, lakini sasa imekuwa sivyo kwani kazi ya ziada inabidi ifanyike.
Lawama ambazo mashabiki wanawatupia wachezaji ni kwa sababu tu wanaamini Stars ilistahili kushinda, lakini walishindwa kujua kuwa hata wachezaji pia walikuwa na akili kuwa watashinda kirahisi.
Soka la sasa hata Stars ikipangiwa na Comoro, Madagascar, na Shelisheli bado yanatakiwa maandalizi ya hali ya juu, pamoja na wachezaji kuingia uwanjani kama vile wanakwenda kucheza dhidi ya Misri, au Ghana, vinginevyo pia tutachemsha. Wakati wenzetu wanawekeza kwenye soka na kupata wachezaji wazuri kila mwaka, bado Watanzania tunacheza na historia ya majina ya nchi kwenye soka.
Kipigo cha mabao 3-0 Cape Verde kiwe somo kwa Watanzania wote kuwa soka duniani limesambaa na kukua kwa kasi, hivyo haipaswi kudharau nchi yoyote ile.