Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amepongeza hatua ya klabu ya AS Monaco kumteua Thierry Henry kuwa kocha mkuu, akisema ni hatua nzuri lakini akimpa onyo kocha huyo kujiandaa dhidi ya shinikizo la kazi.
Thierry Henry ameteuliwa kuwa kocha mpya wa klabu hiyo baada ya kufanya vizuri na timu ya taifa ya Ubelgiji akiwa kama kocha msaidizi, ambapo aliisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka huu.
“ Bila shaka, Henry ni chaguo sahihi, ana kila sifa ya kuwa kocha. Ana maarifa makubwa sana na anaujua vema mchezo wa soka, ndiyo maana ana kila kitu kinachohitajika kwa kila mchezaji kwenye hatua hii ”, amesema Arsene Wenger.
“ Lakini unapoanza kazi hii unahitaji kuwa na bahati, anahitaji kuwa na ari pamoja na kujitoa muhanga maisha yake yote katika kazi hii ”, ameongeza Wenger.
Henry amefanya kazi na Arsene Wenger akiwa mchezaji na kupata mafanikio kadhaa yakiwemo kushinda taji la EPL msimu wa 2003/04, ambapo Arsenal iliweka historia ya kushinda ubingwa huo bila kupoteza mchezo wowote, rekodi ambayo haijafikiwa na klabu yoyote ya ligi hiyo mpaka sasa.
Aliitumikia Monaco katika mwaka 1994 hadi 1999, akiichezea michezo 105 na kufunga mabao 20 kabla ya kujiunga na Juventus na baadaye Arsenal ambako alifundishwa na Arsene Wenger.