Trump Aisuta Saudi Arabia Mauaji ya Mwandishi Jamal Khashoggi
0
October 24, 2018
Rais wa Marekani Donald Trump ameziita harakati za Saudi Arabia kuminya ukweli juu ya mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi kuwa harakati mbaya zaidi katika historia.
Trump pia amesema yeyote aliyesuka mpango huo anatakiwa kuwa katika "matatizo makubwa."
Marekani wamekuwa katika shinikizo la kuwabana washirika wao Saudia juu ya mkasa huo uliotokea kwenye ofisi za ubalozi mdogo wa Saudia jijini,Instanbul Uturuki.
Akiongea na wanahabari katika Ikulu ya White House, Trump amesema: "Walikuwa na wazo duni sana, na wakalitekeleza vibaya mno, na kiufupi harakati zao za kuuminya ukweli ndio mbovu zaidi katika historia ya kujaribu kuficha ukweli."
"Naamini aliyekuja na wazo lile yupo katika matatizo makubwa hivi sasa. Na wanatakiwa kuwa kwenye matatizo," amesisitiza Trump.
Punde tu baada ya kauli ya Trump, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo akatangaza kufutiwa hati za kusafiri za kuingia Marekani kwa watu 21wanaoshukiwa kutekeleza mauaji hayo.
Mamlaka za Saudia zimekuwa zikitoa taarifa za kujikanganya juu ya tukio hilo la kuuwa kwa mwandishi huyo ambaye alikuwa kinara wa kumkosoa Mwanamfalme Mohammad Bin Salman.
Khashoggi, aliingia kwenye ofisi hizo za ubalozi mdogo Oktoba 2 kushughulikia nyaraka za ndoa na hakutoka tena. Awali Saudia walisema alitoka kisha baada ya presha kubwa ya Uturuki na jumuiya ya kimataifa wakakiri aliuawa alipojaribu kupambana.
Hata hivyo, baada ya maswali kuibuliwa na kutaka uchunguzi ufanyike juu ya huo ugomvi uliosababisha Khashoggi kuuawa, Waziri wa Mambo ya Nje ya Saudia Adel al-Jubeir akakiri kuwa Khashoggi ameuawa katika operesheni isiyo rasmi.
Adel al-Jubeir alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News cha Marekani kwamba "mauaji hayo" yalikuwa 'makosa makubwa' na amekana kwamba Mwanamfalme wa Saudia aliagiza mauji hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema nchi yake inafanya uchunguzi huru wa tukio hilo
Katika mkutano na wanahabari ofisini kwake, bwana Pompeo amesema yeye na Rais Trump hawajafurahishwa na yanayoendelea.
"Tunaweka wazi kabisa kuwa Marekani haivumilii kitendo hiki cha kinyama cha kumnyamazisha Khashoggi, mwandishi wa habari,kupitia vurugu," amesema.
Alipoulizwa kama Marekani watakubali maelezo ya Bin Salman kuhusu mkasa huo, Pompeo amesema: "Tutakubali kile tu ambacho Marekani itakigundua."
"Watu wetu wanashughulikia jambo hili katika kila pembe ya dunia ili kuweka uelewa wetu sawa. Tunatengeneza kanzidata yetu wenyewe. Tutafahamu kila kitu sisi wenyewe."
Tags