Tunasukuma Ndani Hadi Jirani- RC Tabora
0
October 31, 2018
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema kuwa kampeni ya 'sukuma ndani' aliyoendesha mkoani humo imesaidia kurudisha watoto wa kike shule kwa asilimia 70 iliyokuwa imetoweka.
Akizungumza kupitia East Africa BreakFast ya East Africa Radio, Mwanri amesema kuwa kampeni ile ilikuwa ikihusika na kuwakamata wote watakaohusika na suala la ndoa za utotoni, wakiwemo washenga na viongozi wa dini lakini kwa sasa wameamua kuongeza na jirani wa familia husika.
Mwanri amesema kazi ya jirani ni kusema mabaya anayoyaona kwa jirani yake ili kuokoa katika masuala yasiyofaa, hivyo endapo jirani atakaa kimya atawajibishwa.
"Watu wengi waliona kuwa natania lakini mimi nilikuwa namaanisha na katika ile orodha ya kusukuma ndani wataoshiriki kumuozesha mwanafunzi tumeongeza na jirani, maana huwezi shuhudia jirani yako anavunja sheria ukaacha kutoa ripoti sehemu inayostahili", amesema Mwanri.
Hivi karibuni Mwanri alisikika akiwaonya wakurugenzi watendaji wa halmashauri, maofisa elimu mkoani Tabora kutimiza wajibu wao, vinginezo atawaondoa baada ya kupokea taarifa kuwa watoto wa kike zaidi ya 11, 000 hawapo shuleni kwa sababu zisizojulikana.
Ndoa za utotoni nchini bado ni tatizo, huku Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na watoto (Unicef), likitoa ripoti kati ya mwaka 2010 na 2017 inayoonyesha Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Sudan Kusini, kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozeshwa ni asilimia 52, Uganda asilimia 40, Tanzania asilimia 31 na Kenya ni asilimia 23.
Tags