Ubao wa Matangazo ulivyozua Kizaa zaa Taifa
0
October 01, 2018
Muda mchache kabla ya kuanza kwa mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, kuliibuka sintofahamu baada ya ubao wa matokeo ya uwanja kuonesha Simba ikiongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga.
Hali hiyo ilendelea hadi muda mchache baada ya mchezo kuanza, hali iliyopelekea mshangao kwa mashabiki hasa wa klabu ya Simba ambao ndio waliokuwa wamekaa katika jukwaa la karibu na ubao huo.
Www.eatv.tv ilipomtafuta Afisa Habari wa shirikisho la soka nchini TFF, Cliford Ndimbo kuzungumzia kuhusu suala hilo kwa upande wao kama wasimamizi wakuu wa mechi, ambapo amesema, " Kwanza hiyo siyo ishu hadi ya kuzungumziwa namna hiyo kwasababu suala hilo limetokea kabla ya mchezo, lingekuwa limetokea katika kipindi cha mchezo ni sawa. Nahisi walikuwa wanajaribu mitambo japokuwa mimi si msemaji wa mmiliki wa uwanja ".
Tukio lingine lililozua sintofahamu katika mchezo huo ni baada ya mwamuzi kupuliza filimbi kuashiria kuanza kwa mchezo, ambapo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib alipiga mpira moja kwa moja hadi nje ya uwanja.
Tukio ambalo wengi wamelizungumzia tofauti, wengine wakilitetea kuwa ni tukio la kawaida katika mchezo wa soka huku wakitolea mifano ya baadhi ya mechi ambazo tukio kama hilo liliwahi kutokea kama mchezo wa Olympic Marseille na Atletico Madrid katika michuano ya 'Europa League' msimu uliopita.
Lakini wengine wakipinga huku wakilihusisha tukio hilo na mbinu chafu za mchezo hasa za kishirikina, mbinu ambazo hazina uthibitisho wowote wa uhalisia wake kusaidia katika michezo wa soka
Tags