Vigogo Kampuni ya Mabasi ya Mwendokasi Dar (UDART) Waendelea Kusota Rumande
0
October 04, 2018
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linaendelea kuwashikilia wafanyakazi wanane wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART) akiwamo kigogo wa idara wa fedha ambao wanadaiwa kuhusika katika mtandao wa uhujumu wa mapato ya mabasi ya mwendokasi kwa kuchapisha tiketi feki kwa abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa huku wengine 18 wakiachiwa kwa dhamana.
Alisema upelelezi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi.
“Bado tunawashikilia watuhumiwa wanane ambao walishiriki moja kwa moja tukio hilo huku wengine 18 ambao walishiriki kwa mbali tumewapa dhamana wakati tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Mambosasa.
Kamnada Mambosasa alisema, watuhumiwa hao wamefanya kosa hilo la kuhujumu mradi wa Serikali ambao ni wa kitaifa na kimataifa kwa kutaka kufifisha jitihada za Serikali.
“Mradi huu unalitangaza Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla kimataifa hivyo kwenda kinyume na jitihada hizo za serikali ni sawa na uhujumu uchumi, upelelezi unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alisema Mambosasa.
Pamoja na hali hiyo alitoa tahadhari kwa Kampuni ya Udart, kuwa makini wakati wa kutoa ajira na kuwataka kufuata vigezo muhimu ili kuepuka kuajiri watu wasiokuwa na sifa.
Taarifa za kna zinaarifu kuwa wafanyakazi hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi , waliunda mtandao maalumu wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha.
Mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000 na kwa kila safari hulazimika kulipa Sh 650 ukijumlisha kwa idadi hiyo mapato kwa siku yaliyokuwa yanakusanywa hufikia Sh milioni 130,000 ingawa kwa sasa yameshuka.
Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi ya Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikingia katika mifuko ya wajanja.
Tags