Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Dr. Harrison Mwakyembe amesema anaimani na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kitakachocheza na Cape Verde leo na kudai kuwa katika timu zilizopo kundi L hakuna timu ya kukitisha kikosi hicho kwani hata Uganda imetoka nao suluhu kwao.
Akizungumza na Kipenga Xtra Waziri Mwakyembe amesema watanzania wategemee matokeo mazuri kwani wachezaji wote wako fiti na mwalimu Emmanuel Amunike ameridhika na kiwango chao.
''Haiwezekani zamani tulifanya vizuri ila hapa kati kulitokea mdudu gani sijui lakini sasa tumeamua kumuondoa, yalikuwepo mazoea ya ushirikina na kuamini tutashinda kwa bahati nasibu bila maandalizi mazuri vitu ambavyo sasa tumeviondoa'', amesema Mwakyembe.
Mwakyembe ameweka wazi kuwa ameongea na wachezaji na kuwaeleza kuwa hakuna staa mkubwa kuliko Tanzania hivyo kama kuna mchezaji anahisi hivyo basi atumie uwezo wake kushirikiana na wenzake kulipa taifa ushindi.
Stars wako nchini Cape Verde ambalo leo watakuwa na mchezo muhimu wa kuwania kufuzu AFCON 2019 wakikipiga na wenyeji wao. Mchezo huo utaanza 2:00 usiku katika dimba la taifa mjini Praia.