POLISI nchini Zambia wanawashikilia raia wawili wa China wkwa kutoa mafunzo kwa jeshi la mgambo mwishoni mwa wiki. Mmoja wa watu hao alikamatwa Jumamosi na mwingine Jumapili katika mji maarufu kwa watalii nchini humo wa Livingstone.
Mkurugenzi wa shirika la huduma za usalama la Alert Safety Security mjini Livingstone pia anashikiliwa, kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Kusini nchini humo, Bonny Kapeso.
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikitoa mafunzo bila kibali kutoka kwa polisi na kwamba sare wanazotumia zinafanana sana na zile zinazotumiwa na maofisa wa Mamlaka ya Taifa ya Mbuga na Wanyamapori.
Polisi walikamata pia bunduki za rashasha, bastola na risasi. Hata hivyo, kampuni hiyo haijazungumzia kisa hicho wala washukiwa wenyewe. Katika siku za karibuni, kumekuwepo na taarifa kuhusu ushiriki wa raia wa China katika shughuli za usalama nchini Zambia na pia deni la taifa hilo.
Washukiwa
Desemba mwaka jana, maofisa wa polisi nchini Zambia walifutilia mbali mpango wa kuwaajiri raia wanane wa China kuwa polisi wa akiba nchini humo. Walichukua hatua hiyo saa 24 baada ya kuzindua mpango huo kutokana na shutuma kutoka kwa raia.
Maofisa hao wapya walikuwa wamepewa jukumu la kufanya doria mjini Lusaka. Uamuzi huo ulizua hisia kali kutoka kwa raia hususan kutokana na agizo jipya lililotolewa mapema mwaka huo ambalo linapiga marufuku maofisa wa polisi kuoa wageni kutokana na sababu za usalama.
Polisi raia wa China waajiriwa Zambia
Raia wa Zambia wenye uraia wa mataifa mawili pia hawaruhusiwi kujiunga na kikosi cha polisi.
Dickson Jere, ambaye ni wakili, alisema kuwa uteuzi huo ulikiuka katiba ambayo inasema wazi kuwa Mzambia yeyote aliye na uraia wa nchi mbili hawezi kujiunga na idara za usalama. Msemaji wa polisi nchini Zambia, Esther Mwata-Katongo, alitetea uteuzi huo wa polisi akisema kuwa kabla ya wao kuteuliwa walichunguzwa na watafanya kazi chini ya usimamizi wa polisi wa kawaida.