Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando ameshindwa kuulizwa maswali na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana baada ya Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kutokuwepo mahakamani hapo.
Wakili Swai ambaye anaiwakilisha Serikali kwenye kesi hiyo, ilielezwa mahakamani hapo yupo safarini Musoma mkoani Mara kwa shughuli nyingine ya kikazi.
Wakili wa Takukuru, Dismas Muganyizi, alieleza mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa Wakili Swai yupo nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na amekwenda Musoma kwenye majukumu mengine na kuiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo.
Hata hivyo, Tido alitakiwa kuulizwa maswali dhidi ya utetezi alioutoa mahakamani hapo Septemba 20, mwaka huu huku akiongozwa na mawakili wake, Dk. Ramadhani Maleta na Martin Matunda.
Hakimu Shahidi aliridhia ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, ambapo Tido ataanza kuulizwa maswali na upande wa mashtaka dhidi ya utetezi wake.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulileta mashahidi ambao ni pamoja na aliyekua Mkurugenzi wa Shirika hill, Clement Mshana, Ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya na Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa.
Tido alisomewa mashtaka manne likiwamo la kutumia madaraka vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 887.1.