Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Athumani Kihamia amesema kuwa muda wa kufanyika kwa uchaguzi mdogo bado upo hadi miezi kumi na mbili kabla ya Bunge kuvunjwa ambapo kikomo kitakuwa mwezi Julai 2019.
Dkt. Kihamia amesema kuwa kwa mbunge atakayejiuzulu baada ya Julai 2019, hatopata nafasi ya kurudi bungeni tena hadi mwaka 2020 mwaka ambao nchi itakuwa katika uchaguzi mkuu na jimbo litakaa wazi.
“Miezi kumi na mbili kabla ya bunge kuvunjwa ndio haiwezekani kufanyika uchaguzi wa marudio ambapo kwa awamu hii tutakwenda hadi Julai 2019, kwahiyo muda bado upo mwingi”, amesema Dkt. Kihamia.
Usiku wa Septemba 27, aliyekuwa Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha alitangaza kujiuzulu uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kusema kuwa amechukua uamuzi huo kumuunga mkono mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.
Kufuatia kujiuzulu kwa Ryoba Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Oktoba 1, amemuandikia barua Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage na kumtaarifu kuwa amepokea barua kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Serengeti (CHADEMA) kujiuzulu hivyo kuiomba tume kuandaa utaratibu wa kufanyika kwa uchaguzi kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi.
Chacha Marwa Ryoba anakuwa Mbunge wa sita wa vyama vya upinzani kuhamavyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi kwa nia ya kuwaletea wananchi maendeleo akiungana na Maulid Mtolea, Mwita Waitara, Julius Kalanga, Godwin Moleli, Zuberi Kachauka ambae anashiriki kampeni za uchaguzi mdogo jimbo hilo la Liwale kwa tiketi ya CCM.