Wanaume kupimwa VVU nyumba kwa nyumba

Wanaume kupimwa VVU nyumba kwa nyumba
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, imewataka wataalamu wa afya na wadau wengine wanaojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, kuwapima wanaume nyumba kwa nyumba kwa madai kuwa hawajitokezi kwenye vituo vya kupimia afya.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Francis Mtega, alipokuwa anafungua kampeni ya "Furaha yangu, Pima Jitambue Ishi" yenye lengo la kuwahamasisha wanaume kujitokeza na kupima afya zao.

Mtega alisema kupitia kampeni hiyo watafanikiwa kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa kuhakikisha wanatokomeza unyanyapaa na kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi na kufikia 90 tatu kama ilivyoelekezwa katika malengo makuu ya kidunia.

"Alisema 90 ya kwanza ni kuhakikisha watu wote wanaoishi na maambukizi ya VVU wanatambuliwa, 90 ya pili ni kuhakikisha watu wote wenye virusi vya Ukimwi (Waviu), wanaanzishiwa na kubaki kwenye huduma ya matunzo na tiba, 90 ya tatu ni kuhakikisha Waviu wote walioanza dawa wanafikia ufubavu wa VVU," alisema Mtenga.

Aidha, Mtega alisema kuwa halmashauri hiyo, itaongeza umakini katika usimamiaji wa mashirika mbalimbali yanayofanya kazi ya mapambano ya VVU na Ukimwi kwa kuzingatia waliongia.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Godfrey Mwakalila, alisema mpaka sasa jumla ya wanaume 455 wamepima maambukizi ya virusi vya Ukimwi, lengo ni kuwafikia wanaume 2,000 ifikapo Juni 2019.

Alisema katika kutoa huduma ya upimaji wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi, jumla ya vituo 54 tayari vinaendelea kutoa huduma na kwamba asilimia 45 ya wanaume ndiyo wamejitokeza kupima, huku wanawake ikiwa ni asilimia 65.

Mratibu wa kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi wilayani humo, Roman Kessy, alisema katika kudhibiti Ukimwi, wanakaridia kufikia mwishoni mwa mwaka 2019 itakuwa na jumla ya watu wanaoishi na VVU kuwa 18,396 wenye umri kati ya miaka 15-49.

Aliongeza kuwa katika kampeni hiyo wanatarajia kuwapima wateja 31,480, huku akibainisha kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu, jumla ya watu 57,559 walitambua hali zao za maambukizi na kati yao wanaume ni 27,793 na wanawake  29,799.

"Katika upimaji huo jumla ya wateja 2,354 walikutwa na maambukizi ya VVU kati yao wanaume ni 993 na wanawake ni 1,361, lakini hadi sasa watu wanaoisihi na virusi vya Ukimwi waliopo kwenye dawa ni 18,192," alisema Kessy.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Konga) ya Mbarali, Veronica Mkune, alisema changamoto inayowakabili ni usiri uliopindukia hasa kwa viongozi wa serikali hali inayosababisha unyanyapaa na ubaguzi katika jamii.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad