WATU tisa ambao hawajatajwa majina yao kwa sababu za kiuchunguzi, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kuuawa kwa kuchinjwa kwa watoto wawili wa familia moja.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Issack Msengi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Issack Msengi, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mashule, Kata ya Kyamulaile wilayani Bukoba.
Alisema kuwa baada ya watoto hao kutoonekana nyumbani kwao mwishoni mwa wiki, miili yao ilioonekana waliuawa kwa kuchinjwa.
Kamanda Msengi aliyataja majina ya watoto waliouawa kuwa ni Auson Respicius (7), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mashule na Alistidia Respicius (5), mwanafunzi wa chekechea katika shule hiyo.
Alisema watoto hao waliondoka nyumbani kwao Jumapili na kwenda katika maduka ya kijiji hicho na kuwa miili yao ilipatikana siku iliyofuata ikiwa katika shamba la migomba na iligundulika kuwa walikatwa shingo kwa kutumia vitu vyenye ncha kali.
"Mauaji haya yanahusishwa na imani potofu za kishirikina," Kamanda Msengi alisema, "kabla ya hili tukio, bibi wa watoto hawa alituhumiwa kwa uchawi, wananchi wakajichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba.
"Inawezekana tukio hili ni ishara ya kuwataka wahame kijijini hapo."
Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa watoto hao, Respicius John, alisema kuwa Jumapili majira ya saa 10 jioni, aliwaruhusu watoto wake kwenda kutembea katika maduka ya kijiji na watoto wenzao.
Alisema ilipofika saa 12:30 jioni, alipata taarifa kutoka kwa mke wake (mama wa kambo wa watoto hao) kuwa watoto hawajarudi nyumbani na akaanza kufuatilia.
"Nilipofika nyumbani, mke wangu akaenda kuangalia kwa majirani hakuwakuta, tukaanza kuwatafuta, nikaenda kwa mama yangu mkubwa sikuwakuta, ikabidi niende dukani kununua vocha ili nimpigie mama yao mzazi akaniambia hawajaenda kwao, sikuridhika ikabidi niende kufuatilia huko lakini sikuwakuta." alisema.
John aliongeza kuwa baada ya kuwakosa watoto hao kwa mama yao, alikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye alimtaka kumtaarifa mwenyekiti wa kitongoji.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutoonekana kwa watoto hao, mwenyekiti wa kitongoji alipiga ngoma ndipo wanakijiji walipokusanyika na kuanza kuwatafuta bila mafanikio.
"Ilipofika usiku bila kupatikana, mwenyekiti akatutaka twende kulala hadi kesho yake (Jumatatu) asubuni ndipo tuendelee na utafutaji. Ilipofika saa mbili asubuhi tukawakuta wamekwishakufa," alisema.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Deodatus Kinawiro, alifika katika kijiji hicho akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama na kuungana na wananchi katika mazishi ya watoto hao.
“Baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa watoto hawa, polisi walikwenda asubuhi kwa ajili ya kufanya uchunguzi, na baadaye waliruhusu watoto wazikwe tukazika," alisema Kinawiro.
Alisema amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Bukoba (OCD), Babu Sanale, kufanya uchunguzi wa kina katika kijiji hicho na kuhakikisha wahusika wanakamatwa.