Watuhumiwa watatu, raia wa Mali, wamekamatwa eneo la Westlands, jijini Nairobi, Kenya, wakiwa na mabilioni ya fedha feki ambazo ni pamoja na Euro, Dola na Pound, zikiwa zimefichwa katika chumba cha nyumba moja.
Katika chumba kingine, polisi waligundua ngozi ya mnyama na shanga, vitu vinavyoaminika kutumika katika ushirikina.
Polisi walisema mmoja wa watuhumiwa aliwatoroka, lakini mmoja wao, raia wa Mali, anayeaminika kuwa ndiye kiongozi wa uhalifu huo, amekuwa akiishi nchini humo kama mhamiaji kwa miaka kumi.
Mkuu wa kikosi kilichofanya oparesheni hiyo, Musa Yego, alisema watuhumiwa hao ni wahamiaji na wamekuwa wakiendesha vitendo vya utapeli kwa wananchi wa Kenya wakidai kuwatajirisha kupitia ushirikina.
Pamoja na kuwaonya wananchi juu ya utapeli huo, amewataka wote waliofikwa na madhila hayo wafike kuwatambua watuhumiwa.