Wazee Yanga Wampitisha Manji

Wazee Yanga Wampitisha Manji
MTAKOMA! Ndivyo unaweza kusema baada ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji, kumaliza utata uliokuwa umeibuka juu ya muundo wa uchaguzi wa klabu hiyo kwa kuwataka wanachama wahakikishe wanaingia kwenye uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi tu.



Awali, Yanga ilitakiwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wao mkuu kwa mfumo wa kujaza nafasi zilizowazi, lakini baadaye kukatokea mpasuko kwa baadhi ya wanachama hasa Baraza la Wazee wa klabu hiyo kugoma wakitaka ufanyike uchaguzi wa jumla yaani kujaza nafasi zote ikiwemo ya Manji ambaye aliwahi kutangaza kujiuzulu.



Jambo hilo lilizua utata na kujikuta baadhi yao wakipeleka malalamiko kwa Waziri Mwakyembe kwani wanachama wengi walikuwa wanahitajika kumchagua makamu mwenyekiti pekee baada ya Clement Sanga kujiuzulu, pia nafasi ya katibu mkuu na baadhi ya wajumbe wa kamati za utendaji waliojiuzulu zinatakiwa kujazwa.



Chanzo makini ambacho kipo ndani ya kamati ya uchaguzi kililithibitishia Championi Jumamosi kuwa, tayari wameshapitisha maazimio hayo ya uchaguzi kwa kujaza nafasi zilizo wazi na kwamba walikuwa wakisubiri ridhaa ya Waziri Dk.Mwakyembe tu ili watangaze siku maalumu ya uchaguzi jambo ambalo tayari ameshalitatua.



“Juzi Jumatano, tulikuwa katika kikao chetu na Waziri Dk Mwakyembe, ambapo kwa ujumla wetu tukiwa na wale wajumbe wa Baraza la Wazee waliokuwa wamepeleka malalamiko kwake, tulimaliza salama huku jambo likibaki kwa waziri mwenyewe ambaye alisema kuwa tayari ameshazungumza na mwenyekiti wetu Manji na Alhamisi walitarajiwa kukutana tena kwa mara nyingine.



“Lengo la kukutana kwa mara zote hizo lilikuwa ni kujadili wafanye uchaguzi wa aina ipi jambo ambalo sisi na Manji tulishakubaliana tujaze nafasi ila tunashukuru kuwa tayari tumeshamaliza kuandaa kila kitu tunasubiri kutangaza tu siku kwani tayari waziri ameshatoa ruhusa hiyo na kuanzia leo (Ijumaa) tutaingia kwenye kampeni tayari kwa uchaguzi,” kilisema chanzo hicho makini.



Championi lilimtafuta Katibu wa Uchaguzi Yanga, Bakili Makele alisema: “Baada ya kikao cha pande zote mimi nikiwemo, Waziri Mwakyembe na wajumbe wote wa baraza la wazee waliolalamika tuliyamaliza na tunasubiri kauli ya Mwakyembe ili kuona mchakato wake unakuwaje.”



Mkurugenzi wa michezo, Yusuf Singo alipoulizwa naye alisema: “Baada ya kukutana kwenye kikao cha kwanza, utata ulikuwa sehemu mbili, ya kwanza ilikuwa namna ya uchaguzi kufanyika kwa maana ya kuchagua viongozi wote na la pili kadi zitakazotumika.



“Suala la kadi za kufanyia uchaguzi tumekubaliana kadi zote za Benki ya Posta na zile za kawaida zitatumika kwa kuzingatia sheria na kanuni zinavyosema, hivyo baada ya kuzitafsiri vyema nadhani hadi Jumapili (kesho) tunaweza kuwaambia namna sahihi sasa uchaguzi utakavyofanyika.”



Alipotafutwa Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali alisema: “Tulikutana na Waziri Mwakyembe kuhusiana na suala la uchaguzi lakini majibu yote kuhusu mchakato huo yatatolewa kesho Jumamosi (leo).”




Yanga ikiwa chini ya uongozi wa Manji imekuwa ikifanya vizuri kutokana na ‘bosi’ huyo kumwaga ‘mkwanja’ wa kutosha ndani ya timu jambo ambalo lilikuwa likiongeza hamasa kubwa na kujikuta wakitwaa makombe kibao wakati yupo ndani ya uongozi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad