Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha Mabwegere na vijiji saba vya wilaya hiyo na mpango wa utekelezaji wake na kuagiza wote waliohusika kupotosha mipaka ya eneo hilo akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi kuchukuliwa hatua za kisheria.
Lukuvi alitoa agizo hilo jana mkoani Morogoro wakati akikabidhi taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye sasa ni jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacob Mwambegele kwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe kuhusiana na mgogoro wa mipaka ya kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mambegwa, Mbigiri, Dumila, Matongolo na Mfulu vilivyopo Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.
"Wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika process yote ambayo kwa kiasi fulani imeigharimu serikali fedha nyingi na kuipa maumivu serikali katika suala hilo ni lazima wachukuliwe hatua kali" alisema Lukuvi.
Taarifa ya uchunguzi ilibaini chanzo cha mgogoro ni kukosekana ushirikishwaji wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya kijiji cha Mabwegere jambo lililosababisha kijiji kiwe na eneo la ukubwa wa hekta 10, 234 kuliko hata kijiji mama cha Mfulu chenye hekta 1,717 jambo lililothibitishwa na ukweli kwamba mipaka ya kijiji hicho imeingia ndani ya mipaka ya kata tatu za Mbigiri, Msowero, na Kitete ingawa kiutawala kijiji cha Mabwegere kinaratibiwa na kata ya Kitete.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisema wizara haijakifuta kijiji cha Mabwegere bali itaanza kutekeleza mapendekezo ya uchunguzi ya kufuta mipaka ya kijiji hicho ambapo sasa TAMISEMI kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa itatakiwa kuanza mchakato wa kuandaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa njia shirikishi.
Katika taarifa yake, Jaji Jacob Mwambegere alipendekeza kwa nia ya kuboresha utendaji kazi, weledi, maadili na umakini na uwezo wa kulinda na kutunza kumbukumbu katika idara ya Upimaji na Ramani na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi hatua za kinidhamu zichukuliwe ili kuzuia migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Wizara ya Ardhi ilikosea katika zoezi la upimaji wa kijiji cha Mabwegere lakini wilaya ya Kilosa itakuwa na jukumu la kuanza mchakato upya wa uanzishaji wa kijiji hicho.
Alisema, kwa kuwa serikali inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani ni jukumu la Tamisemi kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa kuhakikisha mipaka inaandaliwa upya kwa ajili ya kuanzishwa kijiji upya.
Waziri wa Ardhi alisisitiza kuwa shughuli za binadamu kama vile ufugaji na kilimo hazihusiani na masuala ya mipaka, hivyo wilaya ya Kilosa pamoja na kushughulikia suala la mipaka lazima iandae mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuanza kupendekeza maeneo ya ufugaji kwa vijiji vyote saba na kusisitiza kuwa ni lazima busara itumike katika kushughulikia jambo hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Tamisemi Joseph Kakunda alisema uanzishwaji kijiji cha Mabwegere haukufuata sheria na kuwataka wataalamu kuacha kuwa na nidhamu ya woga na kuzingatia kanuni na sheria katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu itakayochunguza mchakato mzima wa kuanzisha kijiji hicho, na kila atakaebainika kuhusika na uanzishaji wa kijiji hicho kinyume na sheria achukuliwe hatua.
Naye naibu Waziri wa Kilimo Merry Mwanjelwa alisisitiza hatua kuchukuliwa kwa wote waliohusika na kusema katika serikali hii ya awamu ya tano ni lazima kufufua makaburi kwa minajili ya kubaini wote waliohusika kuidanganya serikali.
Taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Mabwegere chenye jumla ya hekta 10,234 na mifugo takriban 24,146 na vijiji jirani katika wilaya ya Kilosa à mbao mara kadhaa ulisababisha vifo vya watu tangu mwaka 2008 lifanyika kwa muda wa siku sitini ambapo uchunguzi wake ulizingatia uanzishwaji, upimaji, utolewaji hati miliki kwa kijiji cha Mabwegere, maeneo yenye mgogoro na hatua zilizokwishachukuliwa juu ya mgogoro huo, uwiano wa ardhi, mifugo na mahitaji mengine ya ardhi pamoja na vyanzo vingine tofauti vya mgogoro.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiambatana na Manaibu waziri Tamisemi Joseph Kakunda na Kilimo Merry Mwanjelwa amekutana na viongozi wa Halmashauri za vijiji hivyo saba na kuwasomea taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani.
Lukuvi amewaeleza wananchi hao kuwa ameikubali taarifa nzima ya uchunguzi kwa kuwa sheria inampa nafasi ya kuikubali au kuikataa taarifa hiyo, hivyo kuikubali kwake ni mwanzo wa utekelezaji wa mapendekezo ya uchunguzi na ndiyo maana aliamua kwenda kuwaeleza ukweli wa suala hilo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi viongozi wa wizara nne za Ardhi, Tamisemi, Kilimo pamoja na wizara ya Uvuvi na Mifugo walikaa pamoja na na kupanga mpango wa utekelezaji uchunguzi huo na namna ya kushughulikia mgogoro baina ya kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani.