WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)lijielekezekatika kubuni teknolojia na mitambo rafiki inayolenga kutatua changamoto za wajasiriamali kulingana na mazingira yao.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za SIDO lakini bado kuna changamoto za wajasiriamali wadogo ambazo lazima zishughulikiwe kwa kasi kubwa ili kufungamanisha shughuli za SIDO na uchumi wa Viwanda
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Oktoba 23, 2018) wakati akifungua Maonesho ya SIDO kitaifa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyakabindi vilivyoko wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na wajasiriamali 500.
Amesema ili kufikia uchumi wa kati inambidi kila Mtanzania mahali alipo afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu. “Tusipoteze wakati kwa kufanya mambo yasiyo na tija. Tuzingatie falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu.”
“Mfano kwa hapa Bariadi, tunatarajia SIDO watuletee teknolojia na mitambo inayoweza kurahisisha ukamuaji wa mafuta yanayotokana na mbegu za alizeti na pamba, kwa Dodoma taknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata zabibu.”
“Kigoma pelekeni teknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata mbegu za michikichi na kwenye maeneo yanayolimwa korosho teknolojia na mitambo ya kubangua korosho na maeneo kama Ilula ambayo yanazalisha nyanya kwa wingi wapate teknolojia na mitambo ya kusindika na kuhifadhi nyanya na mbogamboga.”
Waziri Mkuu amesema ili nchi iweze kupata mafanikio, SIDO inatakiwa iwaunganishe wajasiriamali na taasisi mbalimbali za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu. “Mahitaji ni makubwa hivyo lazima SIDO ishirikiane na taasisi nyingine ikiwemo Baraza la uwezehaji Wananchi Kiuchumi. (NEEC).”
Pia, Waziri Mkuu amewasihi wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo kutumia fursa hiyo kujifunza namna nzuri ya kuboresha viwango vya bidhaa zao na kubadilishana ujuzi na uzoefu, kupanua masoko na kubaini teknolojia zitakazorahisisha uzalishaji wa bidhaa.
‘’Kumbukeni kuwa Serikali ina matarajio makubwa katika sekta ya viwaanda hususan katika kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.’’
Awali, Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali ya washirii wa maonesho hayo yakiwemo ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika sekta ya viwanda na biashara zikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO); Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
Mamlaka ya Vyakula na Dawa (TFDA), Wakala wa Vipimo (WMA); Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan-Trade); Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Balaza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC).
Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi hizo zikikishe zinafanya kazi kwa kushirikiana, ujuzi na weledi mkubwa katika kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuendesha shughuli zao kwa viwango vinavyotakiwa.
“Jukumu la mamlaka za Serikali ni kufundisha, kuwalea na kuwaelekeza wajasiriamali wa kitanzania ili wakue na kuwa wawekezaji wakubwa. Pia kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao.”
Waziri Mkuu Aitaka SIDO Kubuni Teknolojia Rafiki
0
October 24, 2018
Tags