Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka vijana kuacha tabia ya kuchagua kazi na badala yake wachangamkie fursa zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa inayoendeshwa na Serikali ikiwemo ya ujenzi.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme, ujenzi wa barabara, upanuzi wa bandari na ujenzi wa miundombinu ya nishati.
Majaliwa ametoa rai hiyo leo Jumatano Oktoba 24, 2018 wakati wa maadhimisho ya miaka 73 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) ambayo kwa mwaka huu yamebebwa na ujumbe ‘Uwezeshaji wa vijana na ubunifu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu’.
Majaliwa amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya ajira sababu iliyoifanya kuanzisha mikakati mbalimbali ambayo inawajengea uwezo vijana.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha wakala wa ajira, mafunzo ya kazi kwa vijana na sera ya ajira.
Amesema pamoja na mikakati hiyo bado kuna changamoto ya ajira hivyo ameiomba UN kuwapa nafasi za ajira, mafunzo kwa vitendo na fursa za kujitolea zinapojitokeza.
Awali, alipowasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam yalipofanyikia maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alikagua gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Waziri Mkuu Awaasa Vijana Kuacha Kuchagua Kazi za Kufanya
0
October 24, 2018
Tags