Yanga Yazungumzia Usajili wa Chirwa

Yanga yazungumzia usajili wa Chirwa
Baada ya Obrey Chirwa kuzua gumzo katika mchezo wa Yanga dhidi ya Alliance Jumamosi hii, Yanga imezungumzia juu ya uwezekano wa kumsajili mshambuliji huyo katika dirisha dogo la Januari.

Chirwa alikuwa miongoni mwa watazamaji wa mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Obrey Chirwa ambaye aliitumikia Yanga misimu miwili kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita akijiunga na klabu ya Nagotoon ya nchini Misri, amekuwa akihusishwa na tetesi za kutaka kurejea Yanga kwa kipindi kirefu kutokana na matatizo ya kutolipwa mshahara katika klabu yake.

Uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika umesema kuwa uwepo wa mchezaji huyo uwanjani haukuwa na uhusiano wowote na usajili wa klabu hiyo na kusisitiza kuwa endapo Yanga itamsajili mchezaji huyo mashabiki watafahamishwa.

"Dirisha la usajili halijafunguliwa, kama Chirwa atakuwa miongoni mwa tutakaowasajili msimu wa usajili utakapofika umma utafahamu. Kuonekana kwake uwanjani hakumaanishi kwamba tupo kwenye mipango ya kumsajili, pengine amekuja mapumziko kuwasalimia rafiki zake", amesema Nyika.

Baada ya matokeo ya ushindi katika mchezo dhidi ya Alliance, Yanga inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara kwa alama 19 baada ya kushuka dimbani michezo saba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad