Yawezekana Masoud Djuma anaondoka kwa kosa lisilomhusu


Na Tom Thomas  
Hatimaye imethibitishwa, Masoud Djuma si kocha wa Simba tena. Yawezekana yalikua ni maamuzi magumu, lakini uongozi wa Simba umeamua kuweka wazi kwamba hawataendelea kufanya naye kazi. Nguvu ya Patrick Aussems imekua kubwa. Yeye ndiye bosi wa bechi la ufundi. Hakuhitaji kufanya kazi na Djuma. 

Walichokifanya viongozi wa Simba ni kumsikiliza bosi wa benchi la ufundi. Patrick Aussems. Pengine kulikua na viongozi waliotamani kumuona Masoud Djuma aliendelea kuifundisha klabu. Pengine kuna viongozi ambao hawakumtaka. Sijui hilo. 

Ninachokifahamu ni kwamba Masoud Djuma alikua kipenzi cha wanachama wengi wa Simba na pengine wapo ambao hawajafurahishwa na maamuzi haya. 

Mimi sijali sana. Ni kitu ambacho tayari kimeshatokea. Kuna kitu nimejifunza kwenye sakata hili. Kitu muhimu sana. Pengine watu wengi hawajakiona lakini ni kitu muhimu sana. Tatizo si la Masoud Djuma wala Patrick Aussems. Tatizo ni viongozi wa Simba. Kwanini? Subiri kwanza twende polepole. Tutaelewana tu. 

November 2015, Masoud Djuma alikua anatambulishwa rasmi kama Kocha msaidizi wa Rayon Sports ya Rwanda. Akimsaidia Mbelgiji, Ivan Minneart. Baadaye mwezi February 2016 Mbelgiji huyu aliamua kuachana na Rayon Sports. Djuma akapata mkataba mpya na kuwa kocha mkuu. 

Nchini Rwanda, Masoud Djuma ni jina linalofahamika sana. Kwanza amezichezea klabu mbili maarufu nchini humo. Rayon Sports na APR. Pili alishinda ubingwa wa Ligi nchini humo kwa rekodi ya aina yake. Akishinda mechi 22, sare michezo saba huku akipoteza mchezo mmoja tu. Mwaka 2017. Akatwaa pia tuzo ya kocha bora wa msimu. 

Alipendwa na kukubalika sana. Yawezekana hata Simba walilisikia sana jina lake. Baada ya Jackson Mayanja kuondoka, akawa chaguo lao la kwanza. Akaletwa nchini kama kocha msaidizi akimsaidia Omog, kisha Pierre Lechantre na baadaye Patrick Aussems. 

Sasa turudi. Tangu Oktoba 2017, Masoud Djuma aliendelea kufanya kazi ileile. Kocha msaidizi. Amekua kocha msaidizi wa makocha watatu. Je hii ni kazi aliyopenda kuifanya? Kumbuka tayari alishakua kocha mkuu wa klabu kubwa nchini Rwanda na kushinda ubingwa. 

Omog aliondoka, Djuma akatajwa kuhusika, Lechantre aliondoka Djuma akatajwa kuhusika. Inasadikika hakuwa na maelewano mazuri na kila aliyekua kocha mkuu. Baadaye akaja Aussems naye inatajwa hakua na maelewano mazuri na Djuma.  

Siku zote ni vigumu kwa makocha wawili wakubwa kukaa ndani ya timu moja. Labda kama wawe marafiki wanaoaelewana. Masoud Djuma anajiamini anaweza kua kocha mkuu. Yawezekana hata mwanzo wakati anasaini mkataba aliminishwa kwamba atakuja kuwa kocha mkuu. 

Hapa ndipo shida ninapoiona. Sioni kama tatizo lilikua ni kwa Masoud Djuma, Omog, Lechantre wala Aussems. Tatizo ni la viongozi wa Simba. Inasadika Djuma hakuaminika kwa viongozi. Hawakumuamini kama anaweza kuwa kocha mkuu. 

Lakini pia kwenye soka la kisasa, anaposajiliwa kocha mpya huja na pendezo la nani anapenda kusaidiana naye. Nani anayehitaji kufanya naye kazi. Hii inatengeneza maelewano mazuri kwenye benchi la ufundi na inatengeneza uimara wa kikosi kwasabu kocha mkuu na wasaidizi wake wanakua sawa kwenye kile wanachokifundisha. 

Jose Mourinho amekua akifanya kazi na Rui Faria tangu wakiwa Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid na Manchester United. Anapofukuzwa kazi Mourinho,Faria anapteza kazi pia. Hata baada ya Faria kuamua mwenyewe kuondoka Manchester United mwezi May mwaka huu, bado Mourinho alimchagua Michael Carrick kuwa msaidizi wake. 

Julai 2016 wakati Pep Guardiola akiwasili Manchester City alimchagua Mikel Arteta awe msaidizi wake. Manuel Pellegrini aliondoka na wasaidizi wake, Guardiola akaja na mtu wake. 

Mapema mwaka huu Zinedine Zidane aliamua kujiuzulu mwenyewe kuifundisha Real Madrid. Yalikua ni maamuzi yake binafsi lakini aliyekua msaidizi wake David Bettoni hakuendelea na kazi yake. Naye aliondoka. Akaja Julien Lopetegui kama kocha mkuu na wasaidizi wake Pablo Sanz na Albert Celades. 

Siku zote kocha mkuu ndiye anayechagua ni nani anayemuhitaji awe msaidizi wake. Viongozi hawamuingilii. Maamuzi yanabaki kwake. Unai Emery alipowasili Arsenal alikuja na msaidizi wake Juan Carlos Carcedo akamfanya Steve Bould kuwa kocha wa kikosi cha kwanza. 

Ni nani aliyetoa pendekezo la Masoud Djuma aletwa Simba kama kocha msaidizi? Wakati ule kocha alikua ni Omog. Je, maamuzi ya kumleta Djuma aje kusaidiana na Omog yalikua ni maamuzi ya Omog mwenyewe? Hata baada ya Lechantre kuwasili je ni yeye aliyemchagua Djuma kama msaidizi wake? Vipi hukusu Aussems? Wakati anajiunga na Simba alihitaji kufanya kazi na Djuma? 

Matokeo yake ndio tunayoyaona Djuma anaondoka kwa kile kinachotajwa 'kutoelewana' kati yake na Kocha mkuu. Kitu ambacho kimeletwa na viongozi kuwakutanisha makocha wawili wasiojuana kufanya kazi pamoja. 

Aussems alikuja Simba akiwa hamfahamu Djuma. Hawakufahamiana. Kwa namna ipi wangeweza kuelewana? 

Yawezekana Aussems alihitaji kufundisha mfumo wake wakati huohuo Djuma alitamani kuona Simba ikiendelea kutumia mfumo wake maarufu wa '3-5-2'. 

Kama viongozi wa Simba walohitaji kocha mpya baada ya Omog au Lechantre kuondoka basi wangemuondoa Djuma mapema. Wangeruhu kocha anayekuja aje na wasaidizi wake na programu zake ili kuepusha huku 'kutoelewana'. 

Lakini pia, tumekua wahanga na makocha wa kigeni. Tunawaamini sana makocha kutoka Ulaya. Bado hatuamini kama kocha mzuri anaweza toka bara la Afrika. 

Masoud Djuma kwa muda mfupi alioifundisha Simba yeye kama Kocha mkuu alifanya vizuri. Alijaribu kuitengeneza Simba mpya na iliyokua imara sana. Hakufanya vibaya. Sikuona sababu ya kutomuamini. 

Kwa kua bado hatuna imani na makocha 'weusi', Simba ilionekana haijakamilika bila kocha wa kizungu. Akaletwa Aussems. 

Sasa Djuma hayupo. Ninachokiona ni mzigo mkubwa anaojaribu kuubeba Aussems. Wengi bado hawana imani nae. Kazi aliyonayo ni kuwafanya wamuamini. Ni kazi kubwa kweli. Anahitaji kupata matokeo kila mechi. Siku ambayo atashindwa kufanya hivyo kelele zitakua kwanini alimuondoa Djuma. 

Si ajabu baada ya muda, Aussems atafanya kazi yake na kuondoka Simba. Kama makocha wengine 'wazungu' wanvyokuja nchini na kuondoka. Yawezekana baadaye Djuma anaweza rudi tena Simba. Ndio, inawezekana. 

0754 896963
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad