Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Jimbo la Kigoma mjini, Zitto Kabwe amefafanua kuhusu sababu za Tanzania kuripotiwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani ilihali wananchi wake wengi wakilalamikia ugumu wa maisha, maarufu kama "vyuma kukaza".
Akizungumza na East Africa Radio asubuhi ya leo Oktoba 17, katika kipindi cha East Africa Breakfast, Zitto amesema kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi, haina maana yoyote kwa mwananchi mmojammoja kwasababu sekta zinazokuwa si zile zinazogusa maisha ya wananchi hao.
"Sekta zinazokua kwa kasi sana hapa nchini ni kama sekta ya mawasiliano na ujenzi, wakati sekta ya kilimo na mifugo inayogusa wananchi wengi ukuaji wake ni chini ya asilimia 4, katika hali hii wanaoweza kuona ukuaji wa uchumi ni watu walio katika sekta hizo tu, ambao ni wachache sana", amesema Zitto.
Zitto ambaye kitaaluma ni mchumi, na aliyewahi kuwa waziri kivuli wa fedha na uchumi katika bunge la 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma, ametoa mifano kuwa miaka ya nyuma nchi za Chad na Guinea ziliwahi kuwa na ukuaji wa uchumi wa asilimia 15 mpaka 20 na zikawa zinaongoza duniani lakini hali hiyo haikuwafanya wananchi wake kuondokana na umasikini wa kutupwa.
"Siku ambayo Tanzania tutafikia asilimia 8 mpaka 10 ya ukuaji wa sekta ya kilimo, ndipo mtaona watu wengi wakiwa na fedha mifukoni." ameongeza Zitto.
Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha siku ya kupinga umaskini ambayo huandhimishwa tarehe 17, Oktoba kila mwaka, ambapo kwa mujibu ya takwimu zilizoripotiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres mwaka 2017, Watu milioni 800 duniani wanaishi na umaskini, huku ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ikiahidi kuhakikisha dunia yenye afya, salama na kujenga jamii iliyo na amani na umoja unaoheshimikwa kwa wote.