20 mbaroni kwa kumteka mwanamke Muitaliano
0
November 25, 2018
Watu 20 wanashikiliwa na jeshi la polisi wakihusishwa na tukio la kumteka mwanamke mmoja, raia wa Italia aliyekuwa anafanya kazi ya kijamii ya kujitolea katika kijiji cha Chakama, Malindi, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, Joseph Boinnet, raia huyo wa kigeni aliyemtaja kwa jina la Silvia Constanca Romano (23), alitekwa Jumanne wiki hii majira ya saa mbili usiku na watu waliokuwa wamejihami na bunduki aina ya AK 47, katika Kituo cha Biashara cha Chamaka.
Amesema kuwa katika utekaji huo, wavamizi walirusha hovyo risasi kuelekea kwa wananchi waliokuwepo ikiwa ni pamoja na eneo walilokuwepo watoto.
“Bado sababu ya watu hao kumteka raia huyo wa kigeni hazijafahamika. Kwa sasa tunawaomba wananchi kutoa taarifa katika kituo chochote cha jirani, punde watakapowaona wahalifu hao pamoja na mwanamke huyo,” IGP Boinnet ameeleza.
Ameongeza kuwa katika tukio hilo la utekaji, watu watano walijeruhiwa wakiwemo watoto. Polisi walifanya msako kwa kutumia helikopta na magari lakini bado hawajampata.
Hata hivyo, jeshi hilo limeeleza kuwa limekamata pikipiki zilizokuwa zimetumika katika uhalifu huo, na limetoa picha za watuhumiwa watatu pamoja na zawadi ya Shilingi milioni 1 za Kenya kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwao.
Mwanamke huyo wa kiitaliano alikuwa anafanya kazi na Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO), la Africa Milele. Shirika hilo lilikuwa linaendelea na mradi wa kuwasaidia watoto yatima ambao wametengwa na jamii, ili kuwawezesha kupata elimu stahiki.
Tags