Klabu ya Arsenal inahofia mshambuliaji wake Danny Welbeck aliumia vibaya wakati wa mechi yao dhidi ya Sporting Lisbon katika kombe la Uropa usiku wa Alhamisi
Mechi hiyo iliyochezewa katika uwanja wa Emirates iliisha bila bao lolote huku Gunners wakijinyakulia nafasi katika kundi la mwisho la timu 32.
Mechi hiyo hata hivyo iligubikwa na tukio la kuumia mguu kwa kiungo wa kimataifa wa England Danny Welbeck.
Meneja wa Arsenal Unai Emery amesema "yuko hospitali''. Tunasubiri matokeo ya uchunguzi wa kimatibabu, lakini tunahisi aliumia vibaya".
Emeri amesema kuwa kila jeraha ni tofauti, lakini huenda Welbeck amevujika sehemu fulani mguuni.
Welbeck aliumia katika dakika ya 25 ya mechi aliporuka na kuangukia vibaya mguu wake wa kulia.
Baadhi ya wachezaji wenzake waliathiriwa sana na ajali hiyo.
"Waliona kwamba ilikuwa ajali mbaya," aliongeza Emery.
"Mchezo wa soka huwa na ushindani mkubwa na ajali kama hizi hatuwezi kuepukana nazo, hungependelea itokee lakini ndio taaluma yetu."
Welbeck amefunga mabao tano msimu huu, pia alichezea England katika mechi yake dhidi ya Uhispania mwezi Septemba ambapo alishirikishwa katika kikosi cha Gareth Southgate.
Kikosi hicho kitacheza mechi ya kirafiki na Marekani pamoja na ligi ya mataifa dhidi ya Croatia.
Mlinzi wa zamani wa Arsenal Martin Keown, amabye sasa ni mchambuzi wa soka wa BT Sport, amesema: "Danny amehusika katika ajali kubwa mbiliakiwa uwanjani''
Aliongeza kuwa huenda mshambulizi huyo wa miaka 27 akaalia nje ya kikosi chake kwa muda.
Meneja wa Arsenal Emery alisema: "Kila mechi tunataka mchezo mzuri kutoka kwa kila mchezaji''.
Aliongeza kuwa Sporting ni timu kubwa, na wachaziji wake wamemakinika. '' Kwa hivyo tulihitaji kuwa waangalifu sana.
Arsenal wanarejea uwanjani tena Jumapili hii katika mchuano wa ligi ya primia watakapokutana na Wolves (16:30 GMT).
Gunners watacheza tena katika ligi ya Uropa Novemba 29 November, ambapo watakuwa wenyeji wa Vorskla Poltava huku Sporting wakichuana dhidi ya Qarabag siku hiyo.