Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 wafanyabiashara wawili kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Katika kesi hiyo, Jamhuri ilikuwa na mashahidi sita na upande wa utetezi washtakiwa walijitetea wenyewe.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shaidi alisema upande wa mashtaka umethibitisha kosa bila kuacha shaka, hivyo mahakama inawatia hatiani washtakiwa kwa mashtaka mawili yanayowakabili.
Washtakiwa waliotiwa hatiani ni Amri Kigahhey, Jairan Rashidi na Ibrahimu Mkande kwa kosa la kuendesha mtandao wa kihalifu na kukutwa na vipande vitano vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 65,640,000.
Tukio hilo lilitokea kati ya Januari 15 na Januari 22 mwaka 2016.
Wakili wa Serikali Elizabeth Mkunde aliiomba mahakama kuwapa adhabu kali washtakiwa kulingana na sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Hakimu Shaidi alisema kwa makosa hayo mawili kila mshtakiwa atakwenda jela miaka 20.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alisema wameridhishwa na hukumu ya mahakama kwani uamuzi huo ni ushindi katika vita ya kupambana na biashara ya nyara za Serikali.