Balozi wa EU nchini Tanzania hajafukuzwa, ameitwa Wakazungumze


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga amesema Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Roeland van de Geer anayeondoka leo usiku Jumamosi Novemba 3, 2018  kurejea kwao, hajafukuzwa bali ameitwa.

Akizungumza na wanahabari jijini Arusha leo Balozi Mahiga amesema de Geer ameitwa katika makao makuu ya umoja huo Brussels, Ubelgiji.

Ametoa kauli hiyo baada ya wanahabari kutaka kujua kama balozi huyo amefukuzwa nchini Tanzania, huku kukiwa na taarifa kuwa ameitwa kujadili masuala ya kisiasa ya hivi karibuni nchini.

“Balozi ameitwa na umoja wa nchi za Ulaya. Kuitwa kwake tumeshauriana na tumejulishwa kwa hiyo amerudi pengine wana jukumu na kazi nyingine,” amesema.

“Ameitwa na amerudi na sisi tumejulishwa kuhusu hilo. Hajafukuzwa ameitwa na shirika lake na mara nyingi vitu kama hivyo hutokea mtu anaitwa na Serikali yake na kupewa majukumu mengine.”

Amesema Serikali imekuwa ikifanya nao kazi vizuri na kushauriana sambamba na kupeana taarifa mbalimbali.

“Kazi ya balozi ni kuwakilisha nchi au shirika lake kama kuna masuala yanahitaji majadiliano na ushirikiano hilo ni lao. Hata mie nilipokuwa balozi niliitwa nyumbani tushauriane na kutoa taarifa na tathmini kuhusu yale niliyotumwa.”

Jana balozi msaidizi, Charles Stuart alisema, “Balozi Roeland ameitwa makao makuu Brussels kwa majadiliano na ngazi za juu za kisiasa wiki ijayo kuhusu matukio ya hivi karibuni.”

Taarifa kutoka ubalozi huo zimeeleza kuwa balozi huyo anatarajiwa kuondoka nchini saa 5:55 usiku leo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad