Mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA), imesema kuwa huduma nyingi kwa sasa zinategemea vitambulisho vya taifa na hayo yanafanyika ili kuongeza msukumo wa watu kufatilia vitambulisho hivyo.
Akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast cha East Africa Radio msemaji wa NIDA, Rose Mdami amesema kuwa mamlaka hiyo inataka kila mtu mwenye umri wa miaka 18 awe na kitambulisho, kwani matumizi yataongezeka zaidi ya hapo.
"Mpaka sasa tumeshaandikisha wananchi milioni 19, na lengo tufike zaidi ya hapo na adhma yetu kila Mtanzania awe na kitambulisho cha taifa ili iwe rahisi kutambuana, lakini pia huduma nyingi za muhimu kwa sasa zinahitaji uwe na kitambulisho cha taifa," amesema Mdami.
Ameongeza kuwa, "Huwezi kuanzisha kampuni bila kitambulisho, huwezi kurudisha kadi ya simu iliyopotea, huwezi muwekea mtu dhamana na itafika mahali hutoweza kufanya chochote nchini kama huna kitambulisho".
Aidha amesema kuwa, suala la kuwa na kitambulisho cha taifa sio la hiari, ni lazima kwa mujibu wa sheria za nchi na havitolewi kwa wazawa tu, hata wageni na wakimbizi pia wanapatiwa ilimradi awe ameishi nchini zaidi ya miezi sita na amefikisha umri wa miaka 18.