Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai amefunguka kuwa bado bunge hilo halijapeleka orodha ya majina ya wabunge pamoja na mawaziri ambao wana mahudhurio hafifu kwenye bungeni ikiwa ni siku chache tangu spika Job Ndugai kutishia kupeleka orodha ya majina hayo kwenye vyama husika.
Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge mara baada ya Spika kutangaza orodha hiyo kazi inayofuata ni utekelezaji wa maagizo hayo ambapo kwa sasa ofisi ya katibu ipo kwenye mchakato kumalizia kupeleka majina hayo.
Akizungumza na www.eatv.tv Stephen Kagaigai amesema “bado suala hilo, linashughulikiwa, na yatap[elekwa majina yote kama ambavyo spikaaliyataja bungeni na kama spika alishasema kilichobaki ni utekelezaji kwetu kwa hiyo wasubiri tu.”
www.eatv.tv pia ilizungumza na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally, juu ya hatua ya kutajwa kwa orodha ya mawaziri na wabunge wa chama hicho ambao ni watoro bungeni, amesema suala hilo atalijibu Katibu wa itikadi na uenezi na Humphrey Polepole kwa kuwa liko chini ya idara yake.
“Maswali ya kuhusu madai hayo ya bunge ni ya idara ya itikadi na uenezi kupitia Humphrey Polepole ambaye kwa sasa yuko Namibia anaweza kurudi leo au kesho mtafute maana hilo swala liko chini ya idara yake” Amesema Dkt. Bashiru Ally.
Novemba 15 Spika wa Bunge Job Ndugai alifunguka orodha ya wabunge na mawaziri ambao wamekuwa na hudhurio hafifu ambapo alitajwa Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje Augustine Mahiga, Waziri wa mazingira January Makamba, pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.